NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
BARABARA kadhaa za Jiji la Arusha ikiwemo Barabara Kuu ya Arusha- Moshi zimefungwa kwa muda kupisha mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amewasili saa tano katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Hata hivyo, wakati barabara zikifungwa mamia ya waendesha bodaboda na magari ya wafuasi wa Chadema walikuwa tayari barabarani nao wakielekea Uwanja wa Ndege wa KIA kumpokea Godbless Lema ambaye anawasili Tanzania leo Machi Mosi.
Askari wa Usalama barabarani wanapata wakati mgumu kuzuia makundi ya bodaboda ambao wamevaa bendera za Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuelekea KIA na magari kadhaa yenye bendera.
Wakizungumza na Demokrasia wakiwa eneo la Maji ya Chai wilayani Arumeru, baadhi ya madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda na magari waliomba ratiba za ujio wa viongozi kuwa wazi.
Mmoja wa madereva hao ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema Lema alitangaza takriban mwezi mzima kuwa leo anarudi, hivyo ili kuondoa usumbufu ratiba za viongozi zingetazama muda wa kufika Arusha ili kuepusha foleni.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya ujio wa Lema, Aman Golugwa amesema ujio wa Rais leo hautaathiri mapokezi ya Lema.
“Tunataarifa kuwa Rais anakuja leo Arusha na sisi tunaendelea na ratiba zetu hatudhani kama kutathiri kitu,” amesema.
Aliyekuwa mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo saa 6:30 mchana akitokea nchini Canada alipokuwa akiishi tangu mwaka 2020.