NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kupanda kwa bei ya petroli na dizeli huku mafuta ya taa yakiadimika.
Kuadimika kwa mafuta ya taa kumesababishwa na uhifadhi wa mafuta hayo kusalia katika Bandari ya Dar es Salaam pekee.
Sambamba na kuadimika kwa mafuta ya taa lakini pia bei ya mafuta ya dizeli imetangazwa kupanda ambapo bei ya mafuta ya Petroli itauzwa Sh.2,960 mwezi huu ikilinganishwa na Sh.2,819 ya mwezi Februari.
Hali kadhalika, bei ya dizeli imeongezeka kidogo kutoka Sh3,105 Februari hadi Sh3,130 mwezi huu sawa na ongezeko la Sh.25.
Wakati bei hizo zikipaa katika jiji la Dar es Salaam, hali ni tofauti kwa mikoa ya kaskazini ikijumuisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambao mafuta ya dizeli yamepungua kwa Sh.64 kwa lita kutoka Sh.2,967 Februari hadi Sh.2,903 mwezi huu.
Huku kwa upande wa dizeli kwenye mikoa hiyo imeshuka kwa Sh209 kutoka Sh3,340 Februari hadi Sh.3,131 mwezi huu.
Utofauti wa bei katika mikoa inasababishwa na umbali wa usafirishaji wa mafuta kutoka bandarini na bandari ambayo mkoa husika unachukua mafuta hayo.
Bei ya mafuta ya taa imeongezeka kwa wastani wa Sh.39 kwa mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga mwezi Machi ikilinganishwa na Februari 2023, huku uhaba wa bidhaa hiyo ukitawala.
Katika taarifa ya bei mpya za mafuta iliyotolewa leo Machi Mosi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Mwainyekule imeonyesha kuisha kwa bidhaa hiyo katika matanki yaliyopo Tanga.
“Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imeonesha katika bandari tatu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zinazopokea mafuta ni mbili pekee (Tanga na Dar es Salaam) ndio zenye matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa.
Kutokana na kuisha kwa mafuta ya Tanga katika Bandari ya Tanga, hivyo nchi nzima kwa sasa inategemea mafuta ya taa kutoka Bandari ya Dar es Salaam huku athari ya kuongezeka kwa bei ya mafuta hayo imeongezeka.
“Bei ya mafuta ya taa mkoani Tanga imeongezeka kutoka Sh.3,107 Februari hadi Sh.3,144 Machi, huku Mtwara ikiongezeka kutoka Sh.3,134 hadi Sh.3,170 mwezi huu,” imesema taarifa hiyo.
Wakati mafuta ya taa yakipatikana katika bandari moja pekee, takwimu za ripoti ya mwisho wa mwaka ya Ewura inaonyesha kupungua kwa uagizaji wa mafuta ya taa kwa asilimia 28 mwaka 2020/2021 ikilinganishwa na mwaka 2019/2020.
“Mwaka 2019/2020 lita 38.47 milioni yaliingia nchini kabla ya kupungua Hadi lita milioni 27.86 kwa mwaka 2020/2021,” ripoti ya Ewura ya Mwaka 2021 imeonyesha.