NA REBECA DUWE , TANGA
ZAIDI ya wakazi 30, 000 katika wilaya tano za mkoa wa Tanga wanatarajia kunufaika na miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mkoa wa Tanga.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Upendo Lugongo ambaye ni meneja wa Ruwasa mkoa wa Tanga wakati akitoa ripoti ya miradi ya maji katika hafla ya utiaji saini mikataba mipya minane iliyogharimu zaidi sh.bil 10/-
Aidha amesema kuwa miradi hiyo ina jumla ya vituo vya kuchotea maji 92 na matangi tisa yenye jumla ya mita za ujazo 1,830 na mtandao wa mabomba kilometa 168.2 ambayo inategemea kuongeza hali ya upatikanaji wa maji wa huduma ya maji kwa asilimia 1.5 kwa wananchi wanaoishi vijijini ambayo itaruhusu maunganisho ya maji majumbani.
Ameongeza kuwa lengo la kusaini mikataba hiyo ni kuingia makubaliano ya pamoja na wakandarasi ambayo yataleta ufanisi na tija ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kufuata kanuni ,taratibu na sheria mbalimbali zitakazofuatwa kwa nia ya kukamilisha utekelezaji huo.
Sambamba na hayo alieleza kuwa katika wilaya hizo tano wilaya Kilindi inatekeleza ujenzi wa mradi maji kwa Maligwa /Gitu na mkandarasi Nipo Africa Engineering Co.limited ambapo katika wilya ya Handeni ni ujenzi wa mradi wa maji Gole mkandarasi ni Lukedan Campaign Ltd.
“Miradi mingine ni upanuzi wa Kwadoya inatelekezwa mkandarasi Wraptec Engineering Limited wilayani Handeni,ambapo wilaya Mkinga mradi wa kufanya utafiti kuchimba visima vitatu katika vijiji vya Mabuta,Mwakijembe na Horohoro. “
Aidha Mhandisi Lugongo amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika utunzaji wa vyanzo maji na kuhakikisha miradi inayojengwa kuepuka kuharibu miundo mbinu ya mradi kwa shughuli za kibinadamu.
Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu mkoa wa Tanga Omary Mgumba ameagiza wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira vijijini Ruwasa kusimamia kwa usahihi miradi hiyo iweze kutelezwa kwa wakati.
Aliwataka wakandarasi ambao hawatasimamia kazi zao vizuri na kutokufikia katika kiwango kilichotakiwa hawataweza kuvumiliwa na serikali ya awamu ya sita ambayo ina nia ya kumtua mama ndoo kichwani.