NA ALI LITYAWI, KAHAMA
WIKI kadhaa tangu Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kupitisha makadirio ya bajeti ya sh. Bil.51.8/- huku bilioni 18.2 ikielekezwa katika matengenezo ya miundombinu ya barabara,baadhi ya wakazi wameonesha mashaka ya kero hiyo ya kutotatuliwa
Wakizungumza na Demokrasia kwa nyakati tofauti , wakazi hao kutoka viunga kadhaa vya Manispaa hiyo, walionesha hofu ya kupatikana Mkandarasi mzalendo atakayetengeneza barabara hizo kwa viwango bora.
Wakazi hao walidai kwa kipindi kirefu kumekuwa na Kero ya miundo mbinu ya barabara katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, licha ya baadhi ya barabara zake kutengewa bajeti ya matengenezo.
” Tatizo ni kupatikana kwa Wakandarasi wenye uwezo wa matengenezo madhubuti ya barabara, ndipo itapunguza changamoto hiyo, kwani imekuwa kawaida barabara hizo kila Mwaka kufanyiwa matengenezo kutokana na kutojengwa kwa ubora, ” amesema Said Hamadi mkazi wa mtaa wa Majengo.
Naye mkazi wa Kata ya Nyadubi, Fundi Abdul, ameeleza kuwa kila mwaka barabara hizo hufanyiwa ukarabati kutokana na mitaa hiyo kutokuwa na mitaro ya kupitisha maji lakini bado miundombinu huharibika pindi inapofika masika.
” Nashangaa kuona wanapitisha kutumia kiasi cha sh.bilioni 18.2 katika bajeti yake ya mwaka 2023/2024 kwa matengenezo ya miundombinu hiyo pasipo mitaro, uimara wa barabara utatoka wapi?, alihoji Fundi Abdul.
Februari 8, mwaka huu, akisoma bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Ofisa Mipango , Flora Sangiwa katika kikao cha baraza la madiwani alisema makisio ya bajeti yote ya mwaka 2023/2023 ya sh.bilioni 51.8 kati ya hizo, kiasi cha sh.18.2 bilioni kipo kwenye miundombinu ya barabara.
Sangiwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 , Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imepanga kukusanya mapato ya ndani kiasi cha sh. bilioni 12.3 huku upande wa mishahara kutumia sh. bilioni 29.2 matumizi ya kawaida sh.bilioni 1.5 na kwenye miradi ya maendeleo itatumia sh. bilioni 8.7
Wakipitisha bajeti hiyo Diwani wa Kata ya Iyenze , Lucas Makulumo , Diwani wa Kata ya Mahengo, Benard Mahongo wamesema wanaunga mkono hoja na madiwani wote wa baraza walipitisha bajeti hiyo.
Katika hoja yake mara baada kupitishwa bajeti hiyo Diwani Mahongo aliomba barabara zitakazofanyiwa matengezo walizozibainisha kuzifanyia matengenezo wazitaje ili wananchi wa maeneo husika waweze kuzifahamu na kujipanga.