NA BARAKA JUMA, MWANZA
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), 1998 – 2013 wilaya ya Sengerema Mwanza Jaji Tasinga amesema kitendo cha serikali ya awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na Rais John Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara ni sawa na nchi kuendeshwa gizani na wananchi hawakujua kilichokuwa kinatendeka serikalini.
Tasinga ameyasema hayo akiwa ofisini kwake wakati alipokuwa akizungumza na Demokrasia kuhusu hali ya siasa hapa nchi na kudai kwamba kwa sasa wananchi wengi hawana simu na hawasomi magazeti na hata kama ni kusikiliza redio na kutazama runinga yanayopatikana ni machache ila kwenye mikutano ya hadhara ujumbe unafika moja kwa moja kwa wananchi.
Ameendelea kwa kusema, serikali inapozuia mikutano ya hadhara ni sawa na kuficha matatizo ya wananchi na kinachobaki ni kusifia tu kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi wa CCM sasa kwa kumsifia Rais Dk Samia Suluhu Hassan wakisema anaupiga mwingi na wakati hali ya uchumi mitaani ni mbaya.
Alidai kuwa wapo baadhi ya wanasiasa na viongozi wapo kwa ajili ya maslahi na kazi yao kubwa ni kumdanganya Rais na si kumueleza ukweli na watu hao wanafanya hivyo kwa kuhofia vyeo vyao kwani wakiusema ukweli huenda wasipate nafasi hizo walizo nazo na hiyo ni aibu kwa taifa.
Tasinga aliendelea “Kwa bahati nzuri umekuja umejionea hali ya hapa kijijini kwetu Nyakarilo hali ya uchumi hapa kwetu tangu uhuru hatujawahi kupata maji, barabara mbovu, vyumba vya madarasa havijitoshelezi na hospitalini watu wanafariki kwa kukosa matatibabu, watumishi wanalia mishahara midogo nikisema hali ya uchumi wetu ni mbaya wala sijakosea” alisema Tasinga.
“Vitu vinapanda bei sana na watu wanaopaswa kumshauri Rais inatakiwa wamueleze ukweli kuhusu ugumu wa maisha mtaani, watu wanakula mlo mmoja kwa siku na watu wamekata tamaa katika nchi yao hii tulivu inayosifika kuwa na amani wakati kila mara watu wanauawa na watu wasio julikana na Jeshi letu limeshindwa kuwakamata watu hao” alisema Tasinga.
Tasinga amedai uchaguzi uliyopita wa chama chake alikuwa nimiongoni mwawagombea wanne waliyomba nafasi ya mwenyekiti CCM Sengerema na mjumbe wa mkutano mkuu na jina lake lilikatwa hapohapo nawala halikufika Dodoma ili lijadiliwe hali aliyoitaja kama hujuma kwake, na anayesema hayo kwa nia njema tu kwani hata katiba ya nchi na CCM inasema, “nitasema kweli daima na fitika kwangu ni mwiko” na ni sehemu ya kufikisha ujumbe kwa Rais kwani watu waliyopewa jukumu la kumshauri wamekuwa wakimdanganya Rais.
Aidha Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kufungulia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kwani kutawasaidia wananchi wengi kujua pale panapovuja na mwenendo wa nchi yao kwa ujumla.