NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwanaume mmoja, mkazi wa Mero, wilaya ya Moshi, mkoani hapa kwa madai ya kumuua mkewe na kumjeruhi mtoto mchanga kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Mwanamke huyo ambaye ametambulika kwa jina la Fausta Tesha (26) aliuawa kwa kukatwa na kisu sehemu za tumboni, kifuani na ubavuni pamoja na kichanga chake usiku wa kumkia februari 23, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Polisi, mtoto huyo mchanga wa wiki mbili amelazwa katika hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu baada ya kuchomwa kisu tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema wanamshikilia mwanaume huyo kutokana na mauaji ya mke wake.
“Mwanaume huyu amemuua mke wake na kumjeruhi mtoto wa wiki mbili kwa wivu wa mapenzi, huyu mwanaume alienda kwenye machimbo huyu mwanamke akawa amepata ujauzito, sasa ikaonekana kuna mgogoro wa familia juu ya huyu mtoto,” amesema.