NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kinahitaji kuiona Zanzibar mpya katika masuala mazima ya kitaifa hasa ustawi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Aidha ACT imesema inahitaji kuona ustawi mzuri wa masuala ya kisiasa kutokana na umakini wao sambamba na kutambua wajibu uliopo mbele yao kutokana na kubeba matumaini ya wananchi.

Kutokana na hayo ndio maana wmekuja na dhamira ambayo ACT ilikaa na kutafakari namna ya kuivusha Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo februari 25 na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Othman Masoud Othman katika uzinduzi wa ahadi za chama kwa wananchi visiwani hapa.
Amesema Zanzibar mpya ni Zanzibar iliyo kitovu cha biashara kwa ukanda wa Afrika mashariki, yenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma za forodha na ufungashaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara.

Ameeleza kuwa Zanzibar Mpya ni Zanzibar isiyo na mfumuko wa bei holelaholela, yenye wananchi wenye kipato cha kutosha kumudu unafuu wa gharama za maisha.
Othman ameeleza kuwa, Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili ni Zanzibar yenye katiba mpya, mifumo bora ya mahakama na utoaji haki, iliyo madhubuti katika vita dhidi ya rushwa.
Makamu Mwenyekiti huyo amekwenda mbali zaidi na kusema Zanzibar Mpya ni Zanzibar iliyoboresha huduma katika utumishi wa umma na mamlaka za serikali za mitaa.

“Zanzibar Mpya ni Zanzibar yenye miundombinu imara na ya kisasa inayopendezesha miji yetu na kuifanya nchi yetu kufanana na miji mikubwa duniani kama ilivyo Singapore, Hongkong na Dubai” amefafanua Othman
Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili ni Zanzibar yenye kuheshimu haki ya wananchi wake katika matumizi ya ardhi, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambazo zitamuwezesha kila mwananchi kumudu makazi ya kisasa.
Pamoja na mambo yote, Othman amesisitiza kuwa Zanzibar Mpya ni Zanzibar yenye watu wenye afya njema, na mifumo bora ya huduma za kinga na matibabu pamoja na hifadhi ya jamii kwa wote.

Ameongeza kuwa, Zanzibar Mpya ni Zanzibar yenye kujitosheleza kwa nishati ya umeme wa uhakika isiyo na athari kwa mazingira na kutoa huduma bora ya maji safi na salama kwa watu wote mijini na vijijini.
“Zanzibar Mpya ni Zanzibar inayotoa elimu bora na bure hadi Chuo Kikuu inayozalisha vijana wenye maarifa na waliojariwa kwenye shughuli za uzalishaji uchumi” amejinasibu Makamu Mwenyekiti huyo
Amebainisha kuwa Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili ni Zanzibar isiyo na ubaguzi katika nyanja zote, yenye umoja, haki, usawa, maridhiano na kuheshimiana. Hii ndio Zanzibar Mpya tunayotaka kuijenga na ndio maana tunafakhari kuja kwenu kuwaambia kuwa tunaweza kuijenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili.

“Sisi ACT Wazalendo, ndicho chombo cha kutufikisha kwenye Zanzibar hiyo, ambayo ni ndoto ya kila mmoja wetu. Ndiyo ndoto aliyotuachia Mzee wetu, Kipenzi chetu, Maalim Seif Sharif Hamad. Sisi, viongozi wa ACT Wazalendo, ndio manahodha wa kukiongoza chombo hiki kufika kwenye lengo la safari hiyo” amefafanua
Aidha ameeleza kuwa Zanzibar haipaswi kuwa kituo cha umasikini uliokithiri, Zanzibar haipaswi kuwa kituo cha vijana waliokosa ajira, Zanzibar haipaswi kuwa kigezo cha nchi yenye huduma mbovu za kijamii, elimu duni, huduma za afya duni.
” Zanzibar imekuwa hivyo kwa sababu ya kukosa viongozi thabiti wenye maono. Sisi katika ACT Wazalendo tunafikiri na tumejipanga kuwa na Zanzibar tofauti na ile Zanzibar iliyozoeleka kwa kipindi cha miaka 60 sasa. Sisi, katika ACT Wazalendo, tunaamini Zanzibar inastahiki kuwa mahala bora zaidi ya ilipo sasa. Na, sisi katika ACT Wazalendo, tunajua namna ya kuifikisha mahala hapo. Ni kwa muktdha huo, ndio maana leo hii tumekuja kwenu kuwaambia mtazamo wetu wa kuijenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili” amesema na kuongeza kuwa

…”Hii ni ahadi (Brand Promise) yetu kwa Wazanzibari, ni mawazo mbadala ya ujenzi wa nchi yetu ili mpate kuyapima na kutupima pia na sisi Viongozi kwa kulinganisha na mawazo ya wengine na mkiridhika mtupe ridhaa ya kuiongoza nchi hii wakati utakapowadia.Mzanzibari mwezangu,Hebu nikuombe mimi nawe tuvute taswira ya kuwa wasafiri na chama ndicho chombo tulichopanda kutufikisha safari hiyo, uongozi wa chama ndio nahodha wa chombo hicho na Zanzibar Njema ndilo lengo la safari yetu.”
Ameendelea kusisitiza kuwa tutazame kila kitu kwenye safari hii: chombo, manahodha, hali za sisi abiria. Chombo chenyewe kiko dhaifu na kinaendeshwa na kwa misingi ya ubaguzi, abiria tumefungwa mikono na miguu hata hatuwezi kufurukuta kutokana na msingi mbovu wa mahusiano kati yake na mshirika mwezake kwenye safari hii. Hapa nakusudia Muungano. Vijana, ambao wengi wa abiria kwenye safari hii hawana uwezo wa kifedha na kiuchumi kuiagharamikia safari yenyewe.
Amejinasibu kuwa wanapokaribia kufika kituo cha safari yao na kukuta Zanzibar si njema tena, bali ni Zanzibar isiyohimilika: gharama za maisha zinazidi kupanda kila uchao, kipato hakiongezeki, miji yake imekosa haiba kutokana na ujenzi holela, huduma mbovu za kijamii, miundombinu mibovu, rushwa imetamalaki kila kona, haki haijuilikani, watu wake wamekuwa kama wanyama, mwenye nguvu ndio mwenye maisha, mnyonge hathaminiwi ni jambo la kustaajabisha.
Ametanabaisha kuwa hii ndiyo safari ambayo Wazanzibari wameienda kama taifa kwa miongo sita mfululizo. Jua, mvua, mchana na usiku. Ndipo chombo na manahodha wake walipowafikisha!Lakini, baada ya miaka 60 ya maisha ya namna hii, sisi abiria wamepata fursa ya kutafakari khatima ya safari yao. Wamesema hapana, hapa sipo walipotaka kuenda. Hawa sio waliotaka wawaongoze kufika lengo la safari yao. Na hiki sicho chombo cha kukipanda kuwafikisha safari hiyo. Wakaamua kwa umoja wao kuwa sasa ni wakati wa mabadiliko na kwa ridhaa yao wakaamua kupanda chombo chengine na kuwapa ridhaa manahodha wa chombo hicho kuongoza safari yao. Chombo hicho kinaitwa MV ACT Wazalendo.
Amesisitiza kuwa Manahodha hao ni wao na viongozi wa chama hicho Safari ya Zanzibar ya Ndotoni kwenye chombo na unahodha wa ACT Wazalendo ikaanza mwaka 2025.
…”Na naam, baada ya miaka 10 matokeo ya safari yako wazi mbele ya macho ya kila abiria. Wametia nanga kwenye Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na Zanzibar yenye Mamlaka Kamili! Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ni Zanzibar yenye nguvu, hadhi na haki kwenye Muungano na Mahusiano ya Maendeleo ya Kimataifa.Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ni Zanzibar yenye sera madhubuti za uchumi na fedha na umiliki kamili wa mafuta na gesi na rasilimali zake zote nyingine”ameeleza Makamu mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa
“Ndugu Wananchi,Niwahakikishie kuwa inawezekana kabisa kuifikisha hapo nchi yetu kuwa na Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili ikiwa tu tunashirikiana na mkitupa ridhaa ifikapo 2025.”