NA MWANDISHI WETU, BURUNDI
WAZIRI wa Fedha na Mipango,Dk Mwigulu Nchemba (Mb) ameshiriki katika Mkutano wa 43 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Bujumbura.
Mkutano huo ambao umefanyika baada ya miaka minane (8) toka ulipofanyika kwa mara ya mwisho nchini Burundi umeshirikisha Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na ushirikiano wa Kikanda pamoja na Mawaziri wenye ajenda zinazojadiliwa na Baraza hilo.
Awali kabla ya Mkutano huo kulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka katika nchi wanachama vilivyofanyika kuanzia februari 19 – 22 Februari, 2023 ambao walipitia ajenda na mapendekezo mbalimbali ya Jumuiya.
Aidha wataalamu hao walipitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo ya biashara, forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira, utawala na fedha.
Dk Nchemba ameshiriki Mkutano huo pamoja na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax (Mb), ambapo watajadili na kupitisha mapendekezo ya ajenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuitangaza lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoa muelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kiswahili na Kifaransa katika uendeshaji wa shughuli rasmi za Jumuiya.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulikuwa chini ya Uenyekiti wa Burundi na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka nchini Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Sudan Kusini umemalizika tarehe februari 23, 2023 na maazimio na ajenda zilizopitishwa zitawasilishwa katika mkutano wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuridhia utekelezaji wake.