NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAKAZI na watumiaji wa Daraja la Kigamboni wanatarajia kunufaika na kifurushi kipya cha Vuka Kidijitali kinachotajwa kusaidia kupunguza gharama za uvukaji katika kivuko hicho .
Aidha kifurushi hicho pia kinadaiwa kitasaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa wavukaji kutokana na kupungua kwa gharama za uvukaji kwa zaidi ya asilimia 70.
Kampeni hiyo imezinduliwa na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Tehama wa NSSF, Donald Mhaiki alisema kampeni hiyo itasaidia kuvuka pasipo kufanya malipo ya fedha tasilimu na kupanga foleni ndefu.
Aidha malipo ya vifurushi yatawapa nafuu watumiaji wa daraja hilo tofauti na awali ambapo watumiaji walikuwa wakitumia zaidi ya sh.90, 000 kwa mwezi lakini kwa sasa watalipia sh. 35, 000 kwa kifurushi cha mwezi.
Mbali ya hayo Mhaiki alifafanua kuwa awali kuvuka kwenye daraja hilo ilikuwa ni lazma ulipie pesa tasilimu kila unapopita lakini hivi sasa utapita bila kikomo kwa gharama ile ile uliyolipia kifurushi cha mwezi au wiki.
Hii ni huduma nafuu sana na unafuu wake unakuja kutokana na vifurushi kupitia kampeni ya Vuka Kidijitali kwa wakazi wa Kigamboni na wengineo ambao hutumia daraja la NSSF Mwalimu Nyerere Kigamboni sasa wataweza kuchagua malipo ya bando la siku ,wiki au mwezi .” alieleza Mhaiki
Kwa upande wake mkazi wa Kigamboni, Naomi Sweya alisema ujio wa Kampeni ya Vuka Kidijitali umemsaidia kumpunguzia gharama kwa karibu asilimia 70 tofauti na hapo awali hivyo anaipngeza NSSF kwa hatua hiyo.