NA MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu hayupo nchini, Demokrasia limebaini.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Lissu ameondoka nchini tangu Jumatano iliyopita, akiwa amekaa nchini kwa siku 21, tangu aliporejea nchini Januari 25 mwaka huu.
Habari zilizoifikia gazeti hili zinasema Lissu amekwenda Ubelgiji alipokuwa anapatiwa matibabu na kuishi tangu Januari 2018.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Singida Mashariki alirejea tena Tanzania Januari 25, 2023 baada ya kujihakikishia usalama wake kufuatia kauli za Serikali zilizowataka wote walioko nje ya nchi kwa sababu za kisiasa warejee nchini.
Lissu alipokelewa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa chama chake na wanachama pamoja na wananchi wengine ambao walimuandalia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Buliaga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Baada ya mkutano huo wa Januari 25, Lissu alipumzika kidogo kwenye makazi yake yaliyopo jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kwao Ikungi, Singida Februari 5.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema alirejea Dar es Salaam kutoka Singida Jumanne, Februari 14 na kesho yake alionekana Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiondoka kwenda nje ya nchi.
Demokrasia lilimtafuta msaidizi wa Tundu Lissu, David Djumbe ambaye alithibitisha kuondoka kwa Tundu Lissu.
“Ndio, mheshimiwa ameondoka nchini na amekwenda Ubelgiji,” alithibitisha Djumbe.
Alipoulizwa kwa nini Lissu ameondoka nchini ikiwa ni wiki tatu tu tangu arudi, Djumbe alisema; “Mheshimiwa amekwenda kwa shughuli zake binafsi pamoja na kuangalia afya yake”.
Djumbe alisema Lissu bado anafanyiwa uangalizi wa afya yake ambapo ana ratiba ya kuonana na jopo la madaktari wake kila baada ya muda fulani.
Kuondoka kwa Lissu kumezua minong’ono hasa ikichukuliwa hivi karibuni baada ya vyombo vya habari vilikuwa vinaripoti kuwa kuna mpasuko ndani ya chama chake.
Vyombo hivyo vya habari likiwemo gazeti moja linalotoka kila wiki liliripoti kuwa kuna pande mbili za Lissu ambaye ni Makamu Mwenyeki na ule upande wa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe unaovutana.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya mvutano baina ya pande hizo mbili ulikanushwa na Lissu wakati akihojiwa na kituo kimoja cha Runinga cha jijini Dar es Salaam.
Gazeti la Demokrasia linafuatilia kwa karibu taarifa hiyo ya kuondoka kwa Lissu na litaripoti kadiri litakavyopata habari.
Lissu aliyeweka makazi yake kwenye mji mdogo wa Tienan, Ubelgiji mara ya kwanza aliondoka nchini usiku Septemba 7, 2017 akitokea Dodoma baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi na watu ambao Jeshi la Polisi liliwaita Wasiojulikana.
Baada ya kuondoka nchini , Lissu alipelekwa nchini Kenya akiwa hajitambui na alilazwa kwenye hospitali ya Nairobi.
Baada ya kupata matibabu kwa miezi minne, mpaka Januari 2018, Lissu alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi.
Juni 26, 2020 mwanasiasa huyo alirejea nchini na chama chake kilimchagua kuwa mgombea nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 ambao chama chake kilikataa kukubali matokeo.
Novemba 5, 2020, Lissu aliondoka nchini kwa msaada wa mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya baada ya mwanasiasa huyo kuomba hifadhi kwenye moja ya balozi hizo akidai maisha yake yalikuwa hatarini.