NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MFUKO wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) umeweka usawa wa ada ya kumuona daktari pamoja kutambua uwepo wa kada ya Madaktari katika ngazi ya afya ya msingi jambo ambalo litawasaidia watanzania kupata huduma bora kupitia mfuko huo.
Aidha imejipanga kufanya maboresho ya kitita cha mafao katika maeneo tofauti ikiwemo kuongeza jumla ya dawa 124 kutoka katika orodha ya dawa muhimu ya Taifa (NEMLIT).
Lengo ni kuondoa changamoto za uandishi wa majina ya baadhi ya vipimo pamoja na kuongeza wigo wa huduma za kibingwa za upasuaji katika hospitali zote za rufaa ya kanda na Taifa.
Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga alipozungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari katika Kikao Kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa maboresho hayo yanakwenda kuleta ahueni kwa wanachama na wadau kwa ujumla ili kuhakikisha wanatoa huduma bora.
Konga alisema kuwa maboresho yamejumuisha dawa zenye nguvu na muundo kwa kuzingatia upatikanaji wa dawa katika soko pamoja na mabadiliko katika ngazi za matumizi ya dawa kama ilivyoanishwa mwongozo wa tiba nchini.
“Katika huduma ya upasuaji na vipimo tutafanya maboresho ambayo yamelenga kwenda sambamba na mapitio ya gharama halisi na uchambuzi wa uhalisia wa bei katika soko” alifafanua Konga.
Alisema kuwa wameweka utaratibu utakaowezesha wanufaika kuzingatia utaratibu wa rufaa, kuongeza huduma zitakazo hitaji uchangiaji (co- payments) na ukomo wa ugharamiaji kwa baadhi ya huduma za makundi ya wanachama.