NA ZUENA MSUYA, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Reli Tanzania (TRC), kutunza Miundombinu ya mradi wa Treni ya Kisasa kwa serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza mradi huo na wao ndiyo wenye dhamana ya kuuendesha na kuusimamia mradi huo.
Kauli hiyo imetolewa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Augustine Vuma wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo ya kukagua chanzo cha umeme wa Gesi Asilia utakaotumika kuendesha treni hiyo ya kisasa katika eneo la Kinyerezi, jana mkoani Dar es Salaam.
Vuma alisema Tanesco na TRC wahakikishe kuwa wanatunza na kulinda mradi huo kwa namna tofauti tofauti ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa endelevu na kuleta tija ilikuyokusudiwa na kwamba Kamati haitegemei kusikia wala kuona miundombinu hiyo inaharibika kwa sababu ya uzembe.
“Wakati Mradi huu unaanza ulikuwa kama ni ndoto, lakini sasa ndoto hiyo imekamilika na mradi huo uko tayari kwa ajili ya matumizi, Kamati imeona nia ya dhati ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kukamilisha miradi mikubwa ambayo iko katika Taifa letu, na imeona nia yake ya dhati ya kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kwa sababu uwekezaji mkubwa katika miradi hii ya uchukuzi ni dhahiri kwamba itawakomboa watanzania kwa kuzingatia usafiri wa Treni ni wa gharama nafuu ukilinganishwa na njia nyingine za usafirishaji hivyo kunyanyua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa kwa ujumla”, alisisitiza Vuma.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wameshukuru kamati hiyo kufika katika eneo la mradi na kwamba wamepokea maelekezo yaliotolewa kuwa kutunza miundombinu kwa kuwa Serikali imetoa fedha nyingi sana kuwekeza katika miundombinu hiyo.
Alisema Tanesco watashirikiana na TRC kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa na kutumia wataalamu wa ndani ambao wamepatiwa mafunzo maalum kutunza miundombinu hiyo kwa weledi mkubwa ili kuwanufaisha watanzania.
Pia aliwataka Watanzania ambao wanaishi pembezoni mwa mradi huo kuendelea kulinda na kuitunza miundombinu hiyo kwa kuzingatia uzio uliowekwa na pia kupita maeneo mahsusi yalioruhusiwa kwa ajili ya usalama wao.
Katika mradi huo kumewekwa utaratibu mzuri wa kuwawezesha Wananchi kupita katika vivuko maalumu ili kuwaruhusu kuendelea na Maisha yao mengine ya kila siku.
Amewahakikishia Watanzania kuwa umeme utakaotumika katika mradi huo ni wa uhakika kutokana na miundombinu thabiti iliyowekwa maalumu kwa ajili ya mradi huo.
“Niwatoe hofu na wasiwasi Watanzania kuwa umeme utakaotumika katika mradi huo utatoka katika vyanzo viwili ambavyo ni umeme wa maji kutoka Kidato, Mtera na Julius Nyerere na ule Gesi Asilia kutoka Kinyerenzi hivyo hakutaweza kutokea changamoto ya umeme, vilevile kuna kila kituo cha umeme kwa kila baada Kilomita 50 ili kufatilia mwenendo wa Umeme katika mradi huo”, alisema Kapinga.
Kamati imezipongeza Tanesco na TRC kwa namna ambavyo wamesimamia ujenzi wa Mradi huo na kukamilika,wameishauri TRC kukamilisha haraka maeneo machache yaliyobaki, na kuhakikisha kuwa mabehewa ya Treni yanakuja na kuanza kutumika kwa sababu miundombinu iko tayari na wameanza majaribio ya kichwa cha treni cha mwendokasi.