NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku nne nchini India yenye lengo la kutanua wigo wa biashara na uwekezaji nchini.
Akizungumzia ziara hiyo leo Oktoba 5, 2023 jijini Dar es salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba amesema ziara hiyo inatarajiwa kuwa yenye tija kubwa kwa nchi kwani mikataba zaidi ya 15 itasainiwa.
Amesema Rais Samia ataondoka nchini Oktoba 8, mwaka huu kwa ziara hiyo na ataongozana na mawaziri wa wizara mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya biashara na uwekezaji inakua nchini.
Makamba amesema ziara hiyo inafanyika kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya India na Tanzania lakini pia ina leno kudumisha na kuendeleza uhusiano katika sekta za kimkakati ikiwemo elimu, maji, kilimo na afya.
Makamba amesema matarajio yanayotegemewa kutokana na ziara hiyo ni pamoja na kuanzisha taasisi ya upandikizaji moyo nchini pamojq na kuanzishwa kwa kiwanda cha chanjo za binadamu na wanyama.
Amesema pamoja na hayo wanatarajia mapinduzi ya kidigitali katika sekta viwanda kwa kuanzisha kiwanda cha kutengenezea simu janja nchini.
Akizungumzia sekta ya kilimo amesema kwenye ziara hiyo inatarajiwa kuja na suluhisho la kudumu la soko la mbaazi nchini India kwani itatoa fursa kwa wakulima kulima zao hilo kibiashara kwani watakua na uhakika wa soko.
“Mbaazi ya Tanzania inaubora sana tutafanya mazungumzo na serikali ya India ili zao hili na mengine yawe na uhakika wa soko India na nchi nyingine.
“Sambamba na hayo katika ziara hiyo wazari wa nchi zote watakutana na kuzungumza namna nzuri ya kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo uwanzishwaji wa kongani ya viwanda” amesema Makamba na kuongeza
“Rais atapata nafasi ya kukutana na wafanyabiasha wakubwa 15 nchini humo ili kuzungumza nao kuhusu kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali,” amesema
Amesema serikali ya India pia itapata fursa ya kuja kuanzisha karakana ya vyombo vya usafiri wa majini hapa nchini.
Hata hivyo amesema wafanyabiashara 80 kutoka hapa nchini wanatarajiwa kwenda kukutana na wafanyabiashara wa India huku Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na ZIPA nao watashiriki ili kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo nchini.