NA MWANDISHI WETU
Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimeyapinga matokeo ya Ubunge yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali, Missana K. Kwangura.
Alizungumza na DEMOKRASIA, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema matokeo hayo ambayo yamempa ushindi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bahati Keneth Ndingo kwa kura 44334 dhidi ya kura 10014 za Modestus Kirufi wa ACT Wazalendo hayakubaliki.
“Uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi sana. Mosi, Msimamizi wa Uchaguzi alivuruga sana zoezi la kuapisha mawakala. Maeneo ambayo aliahidi kuja kuapisha mchana alifika usiku. Hiyo ilisababisha baadhi ya Mawakala wetu na wa vyama vingine wasiapishwe. Lakini hata CCM iliapisha mawakala wachache sana kuliko ACT Wazalendo. Cha kustaajabisha, asubuhi ya siku ya kupiga kura, CCM ilikuwa na mawakala katika vituo vyote.
“Pili, CCM ilitumia vituo ambavyo mawakala wetu walizuiwa kuweka matokeo ya uongo. Ni jambo la kustaajabisha eneo lenye vyumba vitatu, vyumba vyenye mawakala vina mahudhurio hafifu lakini chumba ambacho hakina mawakala kinapewa mahudhurio ya asilimia 100 au zaidi.
“Maombi yetu ya kutaka vituo vyote vyenye utata masunduku yake yahesabiwe upya yalipingwa na Msimamizi wa Uchaguzi. Tunatafakari kuangalia hatua za kuchukua ikiwemo kuyapinga matokeo haya mahakamani” alisema Ado
Katibu mkuu huyo amesema kuwa kasoro zinazojitokeza kwenye chaguzi za marudio zinaitia doa Serikali ya Awamu ya Sita hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
Amesema kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitafanya uchambuzi wa kina wa kasoro zilizojitokeza kwenye Chaguzi zote za marudio na kuandaa Ripoti Maalum itayowasilishwa kwa wadau ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa.
Naye aliyekuwa Mgombea wa Ubunge wa chama hicho, Modestus Dickson Kirufi amesema uchaguzi umekuwa na kasoro nyingi na ni muhimu mamlaka zinazohusika ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi zifanyie kazi kasoro hizo. Pia amesema anasikiliza msimamo wa Chama kujua hatua inayofuata baada ya matokeo kutangazwa.