KARATU, ARUSHA
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antiphas Lissu amekamatwa na Polisi, jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limethinitisha.
Lissu amekamatwa leo asubuhi akiwa hotelini alipofikia eneo la Karatu mkoa wa Arusha.
Jana mwanasiasa huyo aliingia kwenye purukushani na jeshi la polisi baada ya kuzuiwa alipokuwa njiani kuelekea Ngorongoro alipopanga kufanya mikutano ya hadhara.
Baada ya Polisi kuzuia msafara wake, Lissu na pamoja na watu walioambatana nao waliamua kukaa barabarani wakishinikiza kuruhusiwa kuendelea na safari ya kuelekea Ngorongoro.
Leo asubuhi Polisi walivamia hoteli aliyofikia na kutaka waoneshwe chumba alicholala Lissu ambapo baada ya purukushani na walinzi wa mwanasiasa huyo, Polisi walifanikiwa kuingia chumbani kwake na kumkamata yeye pamoja na walinzi na wasaidizi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kumshikilia makamu mwenyekiti huyo wa Chadema.
Kwenye taarifa yake kwa umma, Masejo amesema Jeshi la Polisi linamshikilia Lissu na wenzake kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali na kuwazuia Polisi kutekeleza majukumu yao.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Wakili Welwel alisema pamoja na Lissu, Jeshi hilo linawashikilia mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Suzan Kiwanga na Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Catherine Ruge.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amelaani kitendo hicho akisema sio cha kibinadamu.
Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) Mbowe ameandika yafuatayo; Tunalaani ukamataji, unyanyasaji, usumbufu unaofanywa na Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Dola kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama chetu Mhe Tundu Lissu, viongozi wengine waandamizi wa ngazi mbalimbali, wanachama na wapenzi wetu huko Mkoani Arusha.
“Kwa uzito huo huo, tunalaani uzuiaji wa mikutano yetu na shughuli halali za kisiasa huko Ngorongoro, Loliondo na Karatu. Tuna hofu kubwa ya usalama wa watu wetu na ni dhahiri sasa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inarejesha Utawala wa mabavu usiothamini haki, Uhuru na Demokrasia. Tunafuatilia kwa karibu na tunadai kuachiliwa haraka na bila masharti kwa watu wetu wote!” Ameandika Mbowe