Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimesema kinajipanga vilivyo kwa ajili ya kushinda katika nafasi zote kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025, kwa kuandaa mapema wagombea wenye sifa watakaokiwezesha chama hicho kufikia malengo yake.
Ni miaka 9 sasa imepita tangu Chama hicho cha Siasa kianzishwe mwaka 2014 na tangu wakati huo kimeshiriki katika chaguzi zote huku kikijivunia mafanikio ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo kilipata wabunge wanne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Wabunge wanne wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kufanikiwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar.
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka ujao, kupitia mkutano mkuu wa jimbo la Kigoma Mjini wa kuchagua viongozi wapya, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu, amewataka wanachama wake kupambana kukijenga chama kwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya chama ili kukipeleka chama hicho hatua nyingine.
Katika hatua nyingine Ado amewahakikishia wanachama kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya kisiasa katika kupigania tume huru ya uchaguzi na upatikanaji wa Katiba mpya.
Katibu Mkuu Ndugu Ado Shaibu ameyasema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini uliofanyika jana Juni 11, 2023
OBAMA AJIUNGA NA ACT WAZALENDO.
Asema “Samaki hafundishwi kuogelea”
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji kati ya mwaka 2010 na 2015 kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Issa Hussein Al maarufu ‘Obama’ amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Akizungumza mara tu baada ya kuvalishwa sare ya Chama cha ACT Wazalendo na Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu, Obama ameifananisha hatua ya yeye kujiunga na chama hicho na usajili wa mchezaji mahiri wa mpira.