NA MWANDISHI WETU, TANGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga imeokoa jumla ya Sh milioni 69.5 zilizotokana na mapato ya ushuru katika Halimashauri ya wilaya ya Muheza.
Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa TAKUKURU, Mariam Mayaya wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu Kwa Waandishi wa habari.
Alisema taasisi hiyo ilibaini uwepo wa mtoa huduma za wakala wa makusanyo ya ushuru na maduhuli ya serikali katika Halimashauri ya Muheza akiwa amekusanya fedha pasipo fedha hizo kuingizwa kwenye akaunti ya benki.
“Baada ya uchunguzi tuliweza kubaini wakala huyo amekusanya zaidi ya Sh milioni 83.7 pasipo kuzipeleka benki na ndipo uongozi wa Halimashauri ulipomtaka wakala huyo kuingiza fedha hizo ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kufanikiwa kuingiza Sh milioni 69.5″alisema Mayaya.