NA TATU MOHAMED, DAR ES SALAAM
KATIKA kuadhimisha siku ya Hedhi duniani ambayo hufanyika Mei 28, kila mwaka Shirika la WaterAid Tanzania limetoa msaada katika shule ya sekondari ya Misima iliyopo Wilaya ya Handeni ili kuwasaidia wasichana wanaopata hedhi kuendelea na masomo.
Msaada huo ni cherehani moja kwa ajili ya wanafunzi kujishonea pedi za kitambaa, vifaa 40 vya kushonea pedi, katoni 55 za pedi (kutumika katika kipindi cha mvua pale pedi za kufua zitashindwa kukauka), vifaa vya michezo seti 3, mabango 20 kwa ajili ya kujifunza masuala ya usafi na televisheni kwa ajili ya kujifunza tabia siha na usafi kwa ujumla.
Akizungumza kuhusu Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema katika kuadhimisha siku ya hedhi, wameungana na wanafunzi na walimu katika hafla ya kukabidhi mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji na mafunzo tabia siha uliofadhiliwa na shirika la Hilton Global Foundation pamoja na WaterAid ili kupunguza makali ya ukosefu wa maji katika shule hiyo hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika kipindi cha hedhi.
Amesema pamoja na hayo, wamefanikisha ukarabati wa miundombinu kadhaa ya mfumo wa maji, matenki ya kuhifadhia maji, vyoo ikiwemo kuweka muundombinu wa choo rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Na zaidi ya yote tumeweza kutoa elimu kuhusu usafi kwa wasichana na wavulana katika hatua za makuzi yao binafsi hii ilijumuisha mafunzo maalumu ya namna ya kujitengezea taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi ili kujilinda na adha mbalimbali wanapokua katika kipindi cha hedhi,” amesema Mzinga.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Handeni, Upendo Magashi ameshukuru kwa msaada huo na kusisitiza umuhimu wa kuitunza ili iwasaidie wanafunzi wengi zaidi.
“Miundombinu hii inahitaji kutunzwa ili iweze kutoa huduma husika kwa kipindi kirefu kwa sasa na kwa wanafunzi watakaokuja kusoma katika shule hii hivyo haina budi itunzwe” amesema.
Licha ya kwamba jitihada za dhati zimefanyika na serikali na wadau ila bado inaripotiwa kwamba asilimia 34 ya wasichana hukosa vipindi shule kutokana na upungufu wa vyumba maalumu vya kujisitiri wakati wa hedhi huku asilimia 26 kutokana na ukosefu wa maji na vyoo safi katika shule.
WaterAid ni shirika la kimataifa lenye dira ya kuhakikisha kuwa watu wote ulimwenguni wanapata maji ya uhakika, vyoo bora na huduma za usafi zilizoboreshwa ifikapo mwaka 2030. WaterAid inafanya kazi katika nchi 28, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika.
Nchini Tanzania, shirika la Wateraid lilianza kazi 1983 na kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Maji, Vyoo na Usafi binafsi katika zaidi ya mikoa 11.
Aidha, shirika limeshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni nane wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa miji pamoja na vijijini.