NA MWANDISHI WETU, MVOMERO
TUMBEINE Abdallah (45), ameuawa na tembo usiku wa kuamkia Mei 20 Mwaka huu baada ya kuchomwa na meno ya tembo nyuma ya mgongo wake na mguuni katika kijiji cha Mkata kilichopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, baba mdogo wa marehemu, Paul Saiyuki amesema marehemu ambaye alikuwa ni mfugaji jamii ya Kimaasai alikuwa na wenzake wanne ambapo gafla walipofika jirani na nyumbani kwake walikutana na tembo ambaye alimshambulia na kumsababishia umauti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha mkata, Samson Magao amesema tukio hilo si la kwanza kutokea kijiji hapo, na ameiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwani kijiji hicho kipo jirani na hifadhi ya Taifa Mikumi.
Awali, Ofisa Mhifadhi mkuu hifadhi ya Taifa ya Mikumi kitengo cha Ujirani mwema, David Kadomo amesema watahakikisha wanaendelea na doria ili kudhibiti wanyama hao.