NA MWANDISHI WETU
Klabu ya soka ya Manchester City imetinga fainali ya Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) baada ya kuiadhibu Real Madrid ya Hispania kwa mabao 4-0 jana Jumatano, Mei 17.
Kwenye nusu fainali hiyo ya pili iliyopigwa kwenye dimba la City of Manchester, vinara hao wa ligi kuu Uingereza walikata mzizi wa fitina na kujinyakulia tiketi ya kucheza fainali kwa magoli yaliyofungwa na Bernardo Silva (23,37), Akanji 76 na Alvarez 90+1.
Kwa ushindi huo wa jana, Man City imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa magoli 5-1 baada ya nusu fainali ya kwanza kumalizika kwa kutoshana nguvu ya goli 1-1 mchezo uliochezwa Santiago Bernabeu kwenye jiji la Madrid, Hispania.
Sasa Man City watamenyana na Inter Milan ya Italia kwenye fainali ya mwaka huu baada ya wababe hao wa ligi ya Serie A kutinga fainali kwa kuiondoa AC Milan kwenye nusu fainali ya pili iliyochezwa Jumanne.