NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wa Kariakoo kesho Jumatatu, Mei 15, 2023 watakuwa kwenye mgomo wakiishinikiza Serikali kuwaondolea usumbufu kwenye biashara zao.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakihamasishana kwa kubandika matangazo na kutumia vipaza sauti wakiambiana na kusisitizana kutofungua maduka kuanzia kesho Jumatatu.
Demokrasia imefanikiwa kuona matangazo waliyoyabandika maeneo yote ya Kariakoo yakiwa na ujumbe wa hoja zao.
Matangazo hayo yanasema watakuwa na mgomo usio na kikomo hadi pale serikali itakapoondoa Urasimu bandarini, itakapoacha kutumia askari kukamata hovyo mizigo yao na itakapoboresha sheria mpya ya usajili wa stoo.
Demokrasia linafahamu kuwa wafanyabiashara hao walishawasiliana na kufanya vikao kadhaa na viongozi wa Serikali wakijadili changamoto hizo lakini vikao havikuweza kuzaa matunda.
Vikao hivyo ni pamoja na kile kilichoketi jana Jumamosi kwenye ukumbi wa Karimjee, Posta jijini Dar ambapo uongozi wa wafanyabiashara hao ulikutana na Mkuu wa mkoa, Amos Makalla, viongozi wa Mamlaka ya Kodi (TRA) na wale wa Forodha.
Baada ya kutofika kwenye muafaka, mkuu wa mkoa aliwaomba wafanyabiashara hao wasifunge maduka kesho na badala yake wakutane tena asubuhi.
Wafanyabiashara waligoma ombi hilo la mkuu wa mkoa na kumtaka asifike asubuhi kwani watakuwa kwenye mgomo labda aangalie uwezekano wa kukutana nao kuanzia Saa Saba Mchana.