NA MWANDISHI WETU, DODOMA
KATIKA kudhibiti waajiri wanaonyanyasa na kuwadhulumu wafanyakazi kwa kukwepa kuwapa mikataba na kuwatumia kama vibarua, serikali imetangaza kuanza ukaguzi wa waajiri na watakaobainika watachukuliwa hatua.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi bungeni jana alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda.
Mbunge huyo alieleza kuwa kuna viwanda kwenye Mkoa wa Pwani maeneo ya Mbagala na Mkuranga wanawapa wafanyakazi Sh 4,000 kwa siku.
“Mfanyakazi anaingia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni anapata ujira wa shilingi 4,000 hii ni sawa? Serikali mnasimamia vipi matajiri na waajiri wakubwa ambao wanadaiwa na wafanyakazi madeni ya muda mrefu, kama kampuni ya chai ya Rungwe, mgodi wa Kiwira, Tanesco waliokuwa vibarua takribani sasa ni miaka mitano hawajapata fedha zao,” alihoji.
Akijibu maswali hayo, Katambi alikiri kuwa serikali imebaini kuwapo waajiri wanaokwepa kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi ili kuendelea kuwaita vibarua na kuendelea kufanya nao kazi kwa muda mrefu jambo ambalo ni unyonyaji.
Alisema wameanza kuchukua hatua kwa kufanya kaguzi kujua historia ya wafanyakazi wamefanya kazi kwa kipindi gani na aina ya kazi wanayoifanya ili kuwaingiza kwenye mifumo ya kuwa na mikataba ya kazi na haki zao zilindwe kwa mujibu wa sheria.
Katambi alisema katika sheria ya ajira na mahusiano kazini inaeleza moja ya mambo ni kukubaliana yawe kimkataba na yaandikwe na kuwekwa wazi na kuongeza kuwa kitendo cha waajiri kutolipa mishahara au maslahi yao ni kuvunja sheria ya ajira na mahusiano kazini.
“Ndani ya mkataba kuna masuala ya kodi ya mapato, asipolipa ina maana anakwepa kodi ya serikali na kuna kipengele cha lazima kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, asipolipa mshahara anakwepa pia kupeleka fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na pia kuna kipengele cha mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) kwa hiyo asipolipa mishahara anamkosesha haki mfanyakazi ya kulipwa na tumekuwa tukiwapeleka mahakamani,” alisema.
Katika swali la msingi, Mwakagenda alitaka kujua ni lini serikali itahakikisha Watanzania wanaofanya kazi kwenye kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi ili kulinda haki za wafanyakazi.
Aidha, alisema katika kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, serikali kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara katika sekta binafsi imefanya utafiti na kuboresha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi.
“Viwango hivyo vipya vya mishahara vilitangazwa kupitia Gazeti la Serikali Namba 687 la tarehe 25 Novemba, 2022 na utekelezaji wake umeanza rasmi Januari 1, 2023,” alisema.
Alisema serikali kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya kazi, itaendelea kuhakikisha kuwa waajiri wanatekeleza ipasavyo viwango vya mishahara vilivyotangazwa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya kazi na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili kujenga uelewa wao katika kutekeleza sheria za kazi.
“Ofisi imeendelea kuchukua hatua dhidi ya waajiri wanaobainika kukiuka sheria za kazi hususani ulipaji wa mishahara kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.