NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imetoa Sh bilioni 9.6 kwa Halmashauri na Vijiji vilivyopo pembezoni mwa mapori ya akiba na mapori tengefu zitokanazo na asilimia 25 ya ada ya wanyamapori waliowindwa na utalii wa picha kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2022 hadi Desemba 2022.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Mabula Misungwi Nyanda amesema hayo Mei 10, 2023 akiwa kwenye Ofisi ya Pori la Akiba Kizigo, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, akizungumza na watumishi wakati wa kikazi ya kikazi Kanda ya Kati.
Nyanda amesema uwindaji wa kitalii unaofanyika katika mapori ya akiba na mapori tengefu yanayosimamiwa na mamlaka hiyo umechangia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema umechangia kukuza uchunmi kwa mwananchi mmoja mmoja hususan wale waishio pembezoni mwa mapori hayo.
Hivyo ameupongeza uongozi wa pori hilo na kanda kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwahimiza kuongeza ubunifu, bidii ya kazi ili kuongeza mapato ya Mamlaka na hivyo kuchangia katika pato la Taifa.
“Kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha tuhakikishe tunafanya kazi kwa kujituma, kwa bidii ili kurudisha shukrani kwa Serikali kwa namna inavyotujali” amesema Kamishna Nyanda
Nyanda amewaagiza viongozi na Watumishi wa Kanda hiyo kuhakikisha Vitalu vyote vya Uwindaji wa Kitalii katika Pori la Akiba Kizigo vinapata wawekezaji ikizingatiwa kuwa Pori hilo lina jumla ya Vitalu vinne vya Uwindaji ambapo viwili kati ya vinne vimepata wawekezaji.
Kwa wanyamapori wakali na waharibifu amesema mkazo wa Wizara na Taasisi (TAWA) ni kuhakikisha kuwa adha wanayoipata wananchi kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu inadhibitiwa kikamilifu.
“Hili suala la wanyamapori wakali na waharibifu ni la kupambana nalo usiku na mchana, tupambane kwa nguvu zote na tufanye kila linalowezekana kuhakikisha linadhibitiwa” amesisitiza Kamishna Nyanda
Nyanda amesisitiza suala la viongozi wa vijiji, kata na wilaya kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya matumizi bora ya ardhi kwani wao ndio huwapatia wananchi vibali vya ujenzi na makazi.
Kamishna Nyanda amesema kutokana na kutoelewa huko, wananchi huanzisha kilimo na makazi holela na hivyo kuvamiwa na wanyamapori wakali wakiwemo Tembo.
Nyanda ameelekeza watumishi wa pori hilo kuimarisha mashirikiano na Wadau wa Uhifadhi ili kujenga mahusiano mazuri na kufanya kazi kwa kushirikiana na Wananchi wote wanaozunguka hifadhi hiyo, kwa kufanya hivyo watajenga taswira nzuri ya Taasisi kwa Umma.