NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) wametoa wito kwa watanzania kuendelea kujitokeza na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mpango wa eneo la Soko huru la Afrika (AFCFTA).
Hayo yamebainishawa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi ukuzaji biashara TanTrade, Fortunatus Mhambe na Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA Mwanahamisi Hussein wakati walipokutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa kwanza Tanzania kutoka kampuni ya kizawa ya Export Trading Group (ETG).
Kampuni hiyo imenufaika na mkataba wa eneo huru la biashara Afrika kwa kusafirisha makontena tisa ambazo ni sawa na tani 172.8 za kahawa ya kitanzania aina ya robusta kutoka Tanzania kwenda Algeria na kupata punguzo la kodi la asilimia 23 kupitia cheti cha uasilia wa bidhaa kinachotolewa na TCCIA.
Mhambe amesema, juhudi kubwa zilizofanywa na Rais, Dk. Samia za kuhamasisha uwekezaji na kuimarisha mazingira ya wafanyabiashara nchini zimeleta matokeo chanya katika ukuzaji wa biashara nchini.
Hivyo amesema Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kupitia TanTrade inapenda kutoa wito kwa watanzania wengi zaidi kuendelea kujitokeza na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mpango wa eneo la Soko huru Afrika.
“Napenda kuwahamasisha watanzania kuchangamkia fursa hizo za unafuu wa kodi zinazopatikana katika soko hilo, kwani hii itatusaidia kutokuwa wasindikizaji bali watendaji na walaji wa fursa hizo, hivyo watanzania wengi zaidi wajitokeze TCCIA kuchukua cheti cha uhalisia wa bidhaa.
“Ili kuweza kupata unafuu huo na kupunguza gharama za kodi zitakazowasaidia kuongeza mitaji na kupanua uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla, hivyo kuwasaidia watanzania wengi zaidi kuuza na kutangaza bidhaa zinazozalishwa na Tanzania kwa unafuu zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa TCCIA, Vincent Minja ameongeza kuwa “Kwa mara ya kwanza Tanzania tunatoa cheti cha uasilia kinachomnufaisha mtanzania wa kwanza kufanya biashara katika eneo la Soko Huru Afrika na kupata unafuu wa kodi kwa asilimia 23, kwani alitakiwa achajiwe kodi ya forodha kwa asilimia 35 lakini kupitia cheti cha uhalisia amechajiwa asilimia 12 tu.
“Napenda kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za unafuu wa kodi zinazopatikana katika mkataba huu kwa kuja TCCIA na kuchukua cheti cha uasilia ili kulipa kodi kidogo na kutanua biashara zao,” amesema Minja
Naye mfanyabiashara kutoka katika kampuni ya kizawa ya ETG ambayo imenufaika na mkataba huo, Shaban Fwalo ameishukuru Serikali kupitia TanTrade kwa kuendelea kuwapigia wafanyabiashara na kuwapa elimu kubwa inayosaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara zao.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutufungulia fursa za kurahisisha utendaji wa biashara zetu kuwa nafuu, kwani ilipaswa tulipe kodi ya ushuru wa forodha kwa asilimia 35 lakini kupitia mkataba huu tumelipa asilimia 12, hii itatuletea wateja wengi zaidi kutokana na unafuu wa kodi na itasaidia kupanua soko la bidhaa zetu,” amesema.