NA MWANDISHI WETU, MWANZA
WATU watatu wanaojishughulisha na uvuvi ndani ya Ziwa Victoria wamefariki dunia na wengine watatu kunusurika katika ajali ya mtumbwi iliyotokea katika kijiji cha Nungwe wilayani Geita mkoani hapa.
Ofisa Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Wambura Fidel amethibitisha ajali hiyo leo na kueleza taarifa za ajali walizipokea usiku wa kuamkia Jumatatu.
Amewataja waliofariki ni David Mariatabu Mzula (25), Kamuli Mgogoro (20) na Faustine Cleophace Chibuga (28) wote wakiwa ni wavuvi, wakazi wa kijiji cha Nungwe wilayan Geita mkoani hapa.
“Lakini waliookolewa ni Kulwa Thomas (30), Dickson Alphonce (47) na Dickson Majura (22) hao ndio walioweza kuokolewa tangu jana (Jumapili).
“Walikuwa watu sita kwenye chombo cha uvuvi ambao ni mtumbwi, jana saa 12 jioni waliingia majini kwa ajili ya kufanya shughuli zao za uvuvi, lakini bahati mbaya mtumbwi ulikuwa unaingiza maji.
“Walikuwa wakipambana kuchota maji kuyamwaga lakini kasi ya maji iliyokuwa inaingia ilikuwa ni kubwa, ikilinganisha na kasi ya maji ambayo wao walikuwa wanatoa.”
Amesema wananchi waliokuwa karibu na ene la tukio waliokoa watu watatu baada ya kusikia kelele za kuomba msaada na juhudi za kutafuta wengine watatu ziliendelea na walipatikana wakiwa wamekufa.
Amewataka wamiliki wa vyombo vya uvuvi na usafiri majini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kujiridhisha kiwango cha usalama, kufanya ukarabati pamoja kuweka vifaa vya usalama na uokoaji