NA DENIS SINKONDE, SONGWE
MKAZI wa Kijiji cha Igale, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Semeni Shombe (19) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Iyula kujibu shtaka la kuchinja mbwa na kuuza nyama yake kinyume na sheria.
Imedaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka, Dotto Mwita kuwa Aprili 29, mwaka huu saa 7 mchana, mtuhumiwa huyo alikamatwa katika Kijiji cha Ihowa ambapo alichinja na kuuza nyama ya mbwa kwa ajili ya matumizi ya wanadamu kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 181 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16.
Mshtakiwa huyo amekana shitaka hilo linalomkabili
Kwa upande wake hakimu wa mahakama hiyo Mesia Ernest amesema kesi inayomkabili mshtakiwa ni ya kugushi chakula kwa lengo la kuuza kinyume ma kifungu cha 181 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 huku akijuwa kufanya hivyo ni kosa.
Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 11, 2023 itakapotajwa tena na mshtakiwa ameachiwa kwa dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mtendaji wa kijiji.