NA MWANDISHI WETU, GEITA
MAITI ya binti anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18-20, ambaye hadi sasa hajafahamika jina imekutwa kando mwa barabara Mtaa wa Mwembeni, Kata ya Nyankumbu mjini Geita.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Aprili 25, 2023 na kueleza chanzo cha kifo cha binti huyo hakijafahamika.
Kamanda Berthaneema ameeleza taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema Aprili 24, 2023 majira ya saa1:30 asubuhi ambapo jeshi la polisi liliwasili eneo la tukio na kuchukua mwili huo kwa uchunguzi.
“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi. Kwa hiyo kama jeshi la polisi tunaendelea kutafuta chanzo cha kifo cha huyo mtu.
“Lakini pia ndugu wakijitokeza tutafanya uchunguzi ili tuweze kujua kitu gani kimesababishia kifo chake, mwili ulikutwa pembezoni mwa barabara hauna jeraha, na mpaka sasa hivi ndugu hawajapatikana,” amesema.