NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATU wanne wakazi wa eneo la Mbagala Charambe jijini hapa wamehukumiwa kwenda miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke baada ya kukutwa na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Waliohukumiwa ni Samwel Chacha (20), Haji Ally (24), Athuman Halfan (25) na Sadid Seif (19).
Inadaiwa kubwa Februari 8, 2022 eneo la Charambe kwa Mbiku waliiba Runinga yenye thamani ya Sh.400,000 mali ya Yahama Ngingile kabla na baada ya kufanya wizi huo walimkata na panga kichwani.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Aprili 24, 2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Jimson Mwankenja.
Amesema ametoa hukumu hiyo baada ya washtakiwa hao kutiwa hatiani kwa kosa hilo ambapo Mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka lolote.
“Jamuhuri walikuwa na mashahidi wanne pamoja na vielezo huku upande wa utetezi washtakiwa hao walijitetea wenyewe,”amesema Mwankenja.
Amesema mahakama hiyo imewatia hatiani kwa kifungu cha 287A ya kanuni ya adhabu kwa kuwa kulikuwa na uthibitisho la wizi, wakati wa tukio walitumia silaha aina ya panga na ilielekezwa kwa mtendewa.
Mwankenja amesema Mahakama hiyo imezingatia kifungu cha 287A kinaainisha adhabu pekee ni kifungo cha miaka 30 jela.
Amesema kutokana na kifungu hicho cha sheria Mahakama hiyo imewahukumu washtakiwa wote kifungo cha miaka 30 jela na kama hawajaridhika na maamuzi hayo wakate rufaa katika Mahakama Kuu.