NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais wa Marekani Kamala Harris amewasili nchini Tanzania, tayari kwa kuanza ziara ya siku tatu.
Harris amewasili Tanzania akiwa katika ndege ya Air Force 2, toleo maalum la C-32 ya Boeing 757-200 akitokea Ghana ambako ambako alitumia siku tatu za kwanza za ziara yake barani Afrika.
Ziara hiyo ya kiserikali inatokana na mwaliko wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati walipokutana jijini Washington mwaka 2022, ikitajwa pamoja na mambo mengine kuwa ni kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, sambamba na kuzungumzia maendeleo ya uchumi, mabadiliko ya tabia nchi.
Harris amepokelewa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Saa 5:20 usiku akitokea jijini Accra nchini Ghana.
Makamu huyo wa Rais wa Marekani amepokelewa kwa shangwe na bashasha na wacheza ngoma waliokuwepo katika uwanja huku wakina mama wakirusha kanga zao kwa mbwembwe.
Uwanja huo wa ndege ulipambwa pia na bendera ya Marekani na Tanzania.
Kiongozi huyo wa pili wa juu wa Marekani atafanya ziara yake ya siku tatu nchini ambapo miongoni mwa masuala atakayoyafanya akiwa jijini Dar es Salaam ni mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan Machi, 30.
Baada ya mazungumzo na Rais Samia, mwanasiasa huyo wa kwanza mwanamke kuwa Makamu wa Rais Marekani, atatembelea Makumbusho ya Taifa ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha yao au kujeruhiwa na shambulio la kigaidi la bomu katika Ubalozi wa Marekani mwaka 1998.
Serikali ya Tanzania inatarajia ziara ya Harris itaongeza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili sanjari na kukuza biashara na uwekezaji, kuboresha elimu na afya pamoja na masuala ya utalii.
Marekani ni moja ya mataifa yanayoongoza kwa uwekezaji Tanzania. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki uwekezaji wa Marekani nchini Tanzania ni Dola za Marekani 4.8 bilioni sawa na Sh11.13 trilioni. Miradi ya Marekani imetoa ajira 54,584 nchini jambo lililowaokoa maelfu ya watu na ukosefu wa ajira na dhahama la kukosa fedha za kujikimu.
Hata hivyo, ushirikiano wa kibiashara baina ya Marekani na Tanzania si mkubwa ikilinganishwa na ule wa China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stergomena Tax amesema kuwa baada ya kutembelea Makumbusho ya Taifa, Harris atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association (TSA) anapotarajia kuzungumza na wajasiriamali vijana na wale wanaochipukua (Startups).
Mkutano huo utakuwa ni kete kubwa kwa vijana wa Tanzania wanaosaka fursa za kiuwekezaji katika miradi yao ya kibunifu inayosaka mitaji bila mafanikio.
Baada ya ziara yake nchini Machi 31, kiongozi huyo wa Marekani atakuwa anaelekea nchini Zambia kukamilisha ziara yake hiyo barani Afrika ambayo pia ni matokeo ya ahadi ya Rais wa Marekani Joe Biden wakati wa mkutano na viongozi mbalimbali wa Afrika.
Ziara yake imeanzia Ghana, Tanzania na kisha atamalizia Zambia.