NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amewasilisha ripoti ya Hesabu za Serikali leo Machi 29, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Halmashauri 14 nchini zimepata hati zenye mashaka baada ya ukaguzi huku Ushetu ikipata hati chafu.
Hii ni ripoti ya kwanza tangu Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan aingie Madarakani Machi 2021 kufuatia kifo cha Mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli
Mbali na Halmashauri vipo vyama vya siasa ikiwemo SAU , Demokrasia Makini na Mashirika ya Umma zenye hati zisizoridhisha
Amezitaja Halmashauri zilizopata hati zenye mashaka ni Arusha DC, Babati DC, Bahi DC, Geita DC, Geita DC, Geita TC, Kilindi DC, Mbinga TC, Musoma DC, Nkasi DC, Nyasa DC, Simanjiro DC, Songwe DC, Sumbawanga na Ushetu iliyopata hati mbaya.
Katika vyama vya siasa, Chama cha Sau kilipata hati chafu, Demokrasia Makini, UDP na Chama cha wakulima kilipata hati isiyoridhisha.
Katika mashirika ya umma ni Magazeti ya Serikali, Kampuni ya mbolea, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Nzega, Korogwe na Kyela-Kasumuru, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI) na Shirika la Masoko ya Kariakoo.
“Hizi mbili kwa maana ya Kasumuru na Shirika la Masoko Kariakoo nilishindwa kutoa maoni,” amesema Kichere.
Kwa upande wa Serikali Kuu, wakala wa ufundi na umeme walipata hati mbaya, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tarime daraja C ilipata hati yenye mashaka, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika wote walipata hati zenye mashaka.
Katika vyama vya siasa, Chama cha SAU kilipata hati mbaya, Demokrasia Makini, UMD, UDP vilipata hati zenye mashaka huku Chama cha Wakulima (AFP) alishindwa kutia maoni.
Hati hizo ni kati ya 1,045 zimetolewa ambapo 218 ni za tawala za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, 203 mashirika ya umma, 315 ni serikali kuu, 19 vyama vya siasa na 290 ni za miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh.bil 14.2 na Dola za Kimarekani 14,571 kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi.
Kati ya hati hizo asilimia 90 hati zinazoridhisha ni 1,010, 29 zina shaka, hati mbaya tatu na tatu za kushindwa kutoa maoni.
Wakati ukusanyaji wa mapato kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwa ndiyo nguzo ya uendeshaji wa shughuli za eneo husika, CAG amebaini baadhi ya fedha haziwasilishwi benki baada yakukusanywa.
Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Kichere amesema ukaguzi umebaini kuwa Sh11.07 bilioni hazikuwekwa katika akaunti za benki na wakusanyaji wa mapato kutoka Mamlaka za Serikali za Mtaa 98.
Amebainisha kuwa, hiyo inatokana na ufuatiliaji duni kutofanyika kwa uwasilishaji wa hesabu wa mara kwa mara.
“Mawakala wa ukusanyaji mapato katika mamlaka 10 za Serikali za Mitaa hawakuwasilisha Sh.Bil 4.12 kwenye benki husika,” amesema Kichere.
Amewataka wakurugenzi wa maeneo husika kuhakikisha fedha zote zinawasilishwa na kuwekwa benki kwa mujibu wa sheria.
Amefafanua kuwa, Kati ya fedha hizo Sh.bil 8.4 zilitokana na ukwepaji kodi, huku akieleza kuwa fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hamduni amesema Sh.Bil.2.6 zilidhibitiwa na kurejeshwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyokusudiwa na wananchi waliokuwa wamedhurumiwa katika vyama vya msingi katika mikoa ya Manyara, Rukwa, Katavi, Kigoma, Morogoro, Mtwara, Simiyu, Pwani, Singwe, Tanga na Mwanza.
“Takukuru pia ilifanya uchunguzi na kukamilisha jumla ya majalada 1,188 yakiwemo majalada 16 ya rushwa kubwa. Rushwa kubwa ulihusisha ubadilifu wa fedha za mradi wa mabasi yaendayo haraka ambapo jumla ya Sh.bil 8 ” amesema.
“Ubadhirifu wa fedha za NHIF Sh.bilioni 3 na ubadhirifu wa fedha za NBC Sh.Bil 4.7 “ameeleza Hamduni
Amesema majalada mengine yaliyokamilika ni pamoja na 100 yaliyotokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), majalada manane yaliyohusu ubadhirifu wa fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya (Uviko- 19)