NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI ya Tanzania imethibitisha kuwepo kwa virusi vya homa ya Marburg katika mkoa wa Kagera uliopo Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.
Machi 16, 2023, Wizara ya Afya ilitoa taarifa kwa umma ikieleza uwepo wa ugonjwa ambao haukufahamika mara moja ambao uliwakumba watu mbalimbali.
Japo Serikali ya Tanzania imesema imefanikiwa kuuzuia ugonjwa huo wa ajabu uliosababisha vifo vya watu watano kati ya wanane waliougua wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera, umetambuliwa kuwa ni Marburg.
Taarifa iliyotolewa na Serikali imetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu, Machi 21, 2023 jijini Dar es Salaam imesema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.
Waziri Ummy amesema ugonjwa huo hauna tiba bali hutibiwa kwa dalili husika anazokuwa nazo mtu.
Hadi kufikiwa sasa tangu kuripotiwa ni watu nane ndio wameambukizwa na vifo ni vitano na watatu bado wanaendelea na matibabu. Tumefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu haujatoka nje ya eneo lililokumbwa na ugonjwa huu,” amesema Ummy.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema linajiandaa kutuma timu ya dharura mkoani Kagera ili kufanya uchunguzi zaidi wa magonjwa ya mlipuko kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD).
Dk. Matshidiso Moeti, ambaye ni Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema juhudi za mamlaka za afya za Tanzania kubaini chanzo cha ugonjwa huo ni kielelezo tosha cha dhamira ya dhati ya kukabiliana na mlipuko huo.
Tunafanya kazi na serikali ya Tanzania ya kuongeza kasi ya hatua za kudhibiti na kukomesha kuenea kwa virusi na kumaliza milipuko haraka iwezekanavyo,” alisema Dk. Moeti katika taarifa iliyotolewa Machi 21, 2023.