ALI LITYAWI, KAHAMA
WITO umetolewa kwa walimu na walezi kushirikiana kuwafundisha uzalendo watoto sambamba malezi yenye maadili mema huku wakiwapatia ujasiri wa kupaza sauti kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotendwa katika jamii.
Wito huo ulitolewa na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga (CCM), Santiel Kirumba, aliyesisistitiza kufundishwa kwa uzalendo toka ngazi ya Kaya hadi shuleni, na kudai hatua hiyo itasaidia kuondoa vitendo vya ukatili miongoni mwa jamii.
Akizungumza na walimu wa shule ya Sekondari ya Segese kata ya Segese , Halmashauri ya Msalala alipokwenda kutekeleza ahadi yake Sh.600,000 kwa ajili samani za ofisii na printa moja alizokuwa ameahidi kuisaidia shule hiyo,alisema ukatili utamalizwa kwa jamii kuwa wazalendo.
Kirumba alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa jamii mkoani Shinyanga bado vipo juu na kuwaomba walimu kuwafundisha uzalendo watoto sambamba na kuwajengea watoto ujasiri wa kuweza kupaza sauti pale wanapobaini kufanyiwa vitendo vya kikatili wa kijinsia .
“..Tuwafundishe uzalendo watoto wa kujiamini kupaza sauti wasikae kimya wanapobaini kufanyiwa vitendo vya kikatili hatua itakayosaidia kupunguza matukio hayo,” alisema Kirumba.
Pamoja hayo Mbunge , Kirumba alitimiza ahadi zake katika suala la elimu na pia alitoa kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000 ) kwa kijiji cha Ilogi kata ya Bugarama kwa kuunga mkono nguvu za wananchi walioamua kujenga shule ya msingi ili kupunguza msongamano wa watoto katika shule ya msingi iliyopo ya Bugarama.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Segese Johnmary Zenas alimshukuru , Mbunge kwa kutimiza ahadi yake ya fedha za kununua samani za shule pamoja na printa moja ambayo itawasaidia katika majukumu yao ya kila siku shuleni hapo.