NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KITUO Jumuishi cha Mahakama kilichopo Wilaya ya Temeke jijini Da r es salaam kinachojihusisha na utoaji haki wa masuala ya Kifamilia ndoa, talaka na mirathi , kimeamuru wanasiasa Jesca Kishoa na David Kafulila kuchangia matunzo ya gharama za watoto kwa asilimia 50 kwa 50.
Aidha uamuzi huo umepitishwa Mahakama hiyo februari 20 mwaka huu katika kuvunja rasmi ndoa kati ya wanasiasa Kafulila na Kishoa kupitia shauri la ndoa No 217 ya 2022.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mahakama hiyo kuvunja ndoa baina ya wawili hao huku ikitoa amri kwa mama kubaki na watoto ikiwa ni miaka mitano tangu wanandoa kutengana,
Maombi ya Kishoa aliitaka Mahakama ione ndoa kati yake na Kafulila imevunjika kiasi cha kutorekebishika na kuomba amri ya Mahakama kuvunja ndoa hiyo, mjibu maombi aliwasilisha majibu yake na hakuwa na pingamizi juu ya maombi yaliyopo mahakamani.
Eden Kilatu na Rashid Hussein, mawakili wasomi wamemwakilisha mleta maombi na mjibu maombi mtawalia. Kilatu ameiomba Mahakama itoe hukumu kwa kuzingatia shauri la Joseph Warioba Butiku vs Perucy Muganda Butiku (1987) TLR 1,” alieleza nakala ya hukumu iliyotolewa na Hakimu Mwandamizi Swai.S.O.
Hakimu Swai ameeleza kwa upande wake hana mashaka kuwa ndoa ya wadaawa imevunjika kiasi cha kutorekebishika chini ya kifungu 107 (2) (f) cha sheria ya ndoa.
Kwa msingi huo amri ya kuivunja ndoa na talaka inatolewa, sambamba na hilo, watoto wataishi chini ya uangalizi wa mama yao. Mjibu maombi atakuwa na haki ya kuwaona na kuwa na watoto wake mwishoni mwa juma na vipindi vya likizo za masomo,” ameeleza Hakimu Swai.
Katika hukumu hiyo ameeleza kuwa chini ya kifungu 129 cha Sheria ya Ndoa, mjibu maombi anawajibika kutoa matunzo ya watoto kikamilifu.
Ada za shule zitaendelea kulipwa kwa uwiano linganifu (asilimia 50) kwa kila mzazi katika shule watakazokubaliana pamoja. Hayo ndiyo maamuzi ya Mahakama. Kutokana na asili ya shauri hili hakuna amri ya gharama inatolewa. Imeamuliwa na kuagizwa hivyo,” imeeleza Hakimu Swai.
Ndoa hiyo iliyofungwa Aprili 22, 2014 ilivunjwa rasmi Februari 20, 2023 baada ya wanandoa hao kutengana tangu mwaka 2019 kabla Mahakama ione ndoa hiyo imevunjika kiasi cha kutorekebishika.