NA JANETH JOVIN
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeombwa kutoa bure au kwa gharama nafuu mitungi ya gesi inayowasaidia kupumua kwa saa 24 watoto wenye magonjwa adimu ambao wanasumbuliwa na changamoto ya upumuaji.
Hayo yamenainishwa jijini Dar es Salaam na Sharifa Mbarak mama mzazi wa mtoto Ali Kimara (12) ambaye anasumbuliwa na changamoto ya upumuaji hali inayomfanya kutumia mashine ya umeme kupumua kwa saa 24 au kuwekewa mtungi wa gesi pale umeme unapokatika.
Sharifa ameeleza moja ya changamoto ambazo familia nyingi zenye watoto wenye magonjwa adimu ni gharama kubwa za matibabu hivyo ili kuweza kupunguza makali hayo wanaiomba serikali kuangia namna ya kuweza kutoa bure kwa mitungi hiyo ya gesi kwa ajilo ya kuwasaidia watoto hao kupumua.
“Licha ya kutumia mitungi ya gesi na mashine, unakuta hata bima za afya zina kikomo, siyo kila mtu mwenye watoto kama hawa wanaweza kumudu gharama, tunaiomba sana Serikali kulifikiria hili na itusaidie hasa katika upande huu ya mitungi ndio kilio chetu kikubwa” alisema Sharifa.
Hata hivyo amesema licha ya Serikali kutenge bajeti maalumu kwaajili ya kuwahudumia watoto kama Ali ambao wana magonjwa adimu na wapo maeneo mbalimbali hapa nchini, bado suala hilo halijatekelezwa kwa vitendo.
“Tulisikia kuwa kuna kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya watoto wenye magonjwa adimu lakini hatuoni kama zinachuka chini kutufikia, tunaishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali inazozifanya lakini tunaendelea kuwaomba watusaidie ili kuendelea kurejesha matumaini na furaha kwa watoto hawa,” amesema Sharifa
Sharifa ambaye ni mwajiriwa wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) amesema anatambua kuwa kila mtoto anayo haki ya kupata elimu, kwa kulitambua hilo anawaomba wazazi wenye watoto wenye magonjwa adimu wahakikishe wanapata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.
“Elimu ndio ufunguo wa maisha kwa kulitambua hilo mimi na muwe wangu tulipambana kuhakikisha Ali anasoma akiwa nyumbani kama walivyo watoto wengine,” amesema