NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa ufafanuzi juu ya Habari iliyosambaa katika mitandaoni ya kijamii kuwa “Huduma ya Pace Maker haipo Muhimbili, Wagonjwa wanakufa” kwamba taarifa hiyo siyo ya kweli na ipuuzwe, kwani hakuna mgonjwa aliyekufa kutokana na tatizo la kutokuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri “Pacemaker”.
Kwa mujibu wa taarifa ya JKCI, Taasisi kuwa na upungufu wa Pacemaker kwa muda wa wiki mbili ilitokana na mtoa huduma ya kusambaza vifaa hivyo kuchelewa kuvileta hapa nchini kutoka nchini Uholanzi.
Aidha taarifa hiyo ilibainusha kuwa, iwapo inatokea upungufu wa vifaa hivyo Taasisi ina utaratibu wa kuhifadhi vichache kwa ajili ya kutumika kwa wagonjwa wa dharura kwani wagonjwa wanaowekewa Pacemaker wapo wa aina mbili kuna wa dharura na wale wanaoweza kusubiri.
Kutokana na changamoto hiyo wagonjwa wote waliokuwa wa dharura waliwekewa Pacemaker ambapo kwa wiki ya februari 6-12, 2023 wagonjwa watatu waliwekewa kifaa hicho.
taarifa ilikwenda mbali zaidi na kufafanua kuwa, Wiki ya februai 13-19, 2023 hakukuwa na mgonjwa wa dharura aliyehitaji kuwekewa Pacemaker.
Hata hivyo februari 23, 2023 Taasisi ilipokea Pacemaker kutoka kwa mtoa huduma ya kusambaza vifaa hivyo na siku ya jana wagonjwa watatu waliwekewa kifaa hicho na leo februari 24, 2023 ambapo wagonjwa watano wamewekewa pia wanaohitaji kuwekewa Pacemaker wamepewa taarifa kufika Hospitali.
Aidha, endapo itatokea Taasisi ikaishiwa kabisa Pacemaker ingawa haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, kuna utaratibu ambao umewekwa wa kuazima vifaa hivyo kutoka Hospitali za hapa nchini na Afrika ya Mashariki ambazo zinatoa huduma ya upasuaji wa moyo.
Taasisi imetoa onyo kwa watu waliotoa taarifa hii ya uongo ambayo imezua sintofahamu kwa wananchi pamoja na wagonjwa wetu kuacha mara moja kufanya hivyo.
Aidha taarifa hiyo imesisitiza kuwa iwapo mtu anahitaji kupata ufafanuzi kuhusu huduma zetu au anakutana na changamoto yoyote ile ya kimatibabu afike katika Taasisi yetu au apige simu namba +255688027982 au +255782042019 kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi.