NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kusimamia na kuimarisha mifumo ya malipo nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha kwa urahisi, usalama na ufanisi zaidi.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Lucy Shaidi katika mkutano maalumu wa kuelimisha wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusu matumizi ya mifumo ya malipo ya kielektroniki.
Amesema licha ya kusimamia mifumo hiyo ua malipo nchini,BoT imeweka mkazo katika kuimarisha matumizi ya mifumo rasmi ya malipo ya kielektroniki ili kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kujenga uchumi wa kisasa wenye usalama, ufanisi na ushindani katika shughuli za biashara nchini.
Shaidi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, wa kisasa na wa kipato cha juu, ambapo teknolojia na uchumi wa kidijitali vimetajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo.
Aidha, Shaidi imetoa wito kwa taasisi za kifedha na wadau wengine wanaotoa huduma za malipo kuhakikisha mifumo yao inakuwa imara na yenye uwezo wa kurahisisha miamala kwa wananchi.
“Pamoja na kuendelea kupanua huduma za malipo kwa wananchi, ni muhimu kwa taasisi zinazotoa huduma hizo kuimarisha mifumo yao ili kuhakikisha miamala inafanyika kwa ufanisi,” amesema
Katika hatua nyingine, Shaidi amesisitiza umuhimu wa benki na taasisi za kifedha kuweka wazi gharama za huduma mbalimbali wanazotoa ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kabla ya kutumia huduma hizo.
Ameeleza kuwa tayari kuna zana ya kulinganisha gharama za huduma za benki (Price Comparison Tool), inayowawezesha wananchi kulinganisha ada na gharama za huduma zinazotolewa na benki mbalimbali kabla ya kuchagua huduma wanayoihitaji.
Akizungumzia kuhusu mkutano amesema umelenga kutoa fursa kwa BoT kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mifumo hiyo ili kupata suluhisho na kuboresha huduma za malipo nchini.
“Mkutano huu pia umeandaliwa kutoa nafasi kwa BoT kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mifumo hiyo, ili kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha huduma za malipo nchini,” amesema.
Naye Meneja Msaidizi wa Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa BoT, Fabian Kasore amesema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yamekuwa chachu ya kurahisisha shughuli za biashara kwa kuwawezesha wafanyabiashara kufanya miamala kwa haraka bila kutumia muda mwingi kufuata foleni katika benki ili kupata huduma za kifedha.
Ameeleza kuwa kupitia mifumo hiyo, wafanyabiashara wanaweza kufanya miamala papo hapo, jambo linalochangia kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku.
Aidha, amewapongeza wafanyabiashara kupitia jumuiya yao kwa ushirikiano wao, huku akiwahimiza kuendelea kutoa nafasi za majadiliano ili kuboresha huduma na kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Donath Kibwana, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, ameiomba BoT kuhakikisha mifumo ya malipo ya kidijitali inakuwa huduma yenye gharama nafuu badala ya kuonekana kama njia ya kuongeza mapato.
Amesema wafanyabiashara wanatambua faida za mifumo hiyo, ikiwemo kuwezesha miamala kufanyika papo hapo bila kulazimika kutumia muda kwenda benki kusubiri fedha taslimu, lakini wameomba makato yanayotozwa yaangaliwe kwa kuzingatia viwango vinavyotumika katika nchi nyingine.
Kibwana ametoa mfano wa Kenya, ambako amesema matumizi ya fedha taslimu yamepungua kutokana na kuimarika kwa mifumo ya malipo ya kielektroniki, akisisitiza umuhimu wa Tanzania kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia wafanyabiashara kutumia huduma hizo.
Amesema jumuiya hiyo inathamini nafasi iliyopewa na BoT kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, huku akiiomba benki hiyo kuendeleza vikao vya majadiliano ili kuimarisha mawasiliano, kutatua changamoto na kuweka mazingira bora ya matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.




