NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuandaa mwongozo wa kutekeleza Programu ya Sanaa mtaa kwa mtaa ili kuibua vipaji vingi kuanzia ngazi ya chini.
Chana ametoa maagizo hayo Februari 21, 2023 alipofanya ziara katika Baraza hilo ambapo amesisitiza Sekta ya Sanaa kuendelea kuongeza ukuaji katika Pato la Taifa
“Natoa rai kwenu BASATA kuwa na takwimu sahihi kuhusu idadi ya Wasanii katika aina zote za Sanaa ambazo zitakuwa zinahuishwa kila baada ya muda mfupi na zitasaidia katika upatikanaji wa mikopo pamoja na udhamini kutoka taasisi mbalimbali,”amesema Waziri Chana.
Amesisitiza Baraza hilo kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa Sanaa katika kufanya Sanaa zinazoelimisha, kuburidisha bila kuvunja maadili ya Kitanzania.
Awali, akimkaribisha Waziri, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pauline Gekul amesisitiza Baraza hilo kutoa kipaumbele katika sanaa nyingine kama linavyofanya katika muziki pamoja na kutoa fursa kwa vikundi mbalimbali vya maeneo tofauti kushiriki matamasha ya kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Kedmon Mapana amesema Baraza hilo limefanikiwa kuanzisha mfumo wa usajili wa Wasanii Kidijitali, pamoja na kurejesha Tuzo za Muziki.
Paulina Gekul Naibu Waziri wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo