NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Mahusiano), Dk. Evaline Wilbard amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya ujuzi kwa vijana kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa wataalamu wake wenyewe katika miaka ijayo.
Akizungumza Julai 5, 2026 baada ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, Dk. Wilbard alisema Serikali imeanza kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza ujuzi kwa vijana ili kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.
“Tupo katika dunia inayohitaji ujuzi zaidi. Serikali tayari imeanza programu za maendeleo ya ujuzi kwa vijana, na tunaamini kuwa baada ya miaka michache Tanzania haitalazimika tena kutegemea wataalamu kutoka nje kwa sababu tutakuwa tumewazalisha wenyewe ndani ya nchi,” alisema Dk. Wilbard
Alibainisha kuwa juhudi hizo zinatekelezwa kwa kuzingatia maelekezo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Aidha Dk. Wilbard katika maonesho hayo wananchi wanaopita kwenye banda la Ofisi ya Waziri Mkuu wameendelea kunufaika na elimu kuhusu haki za wafanyakazi, ajira, afya na usalama mahali pa kazi pamoja na huduma mbalimbali za hifadhi ya jamii.
Alisema taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu zimekuwa zikitoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria za kazi, viwango vya chini vya mishahara, afya na usalama kazini, hatua inayochangia kupunguza migogoro, malalamiko na sintofahamu katika maeneo ya kazi.
“Nimefurahishwa na namna watumishi wetu wanavyotoa elimu kwa wananchi kwa weledi mkubwa. Wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali, kueleweshwa na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu kazi, ajira na mahusiano,” alisema.
Kuhusu mahusiano ya kijamii, Dk. Wilbard alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuhimiza mshikamano, umoja na ushirikiano kati ya wananchi, taasisi za dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa kuwa mahusiano bora ni msingi wa maendeleo endelevu.
“Mahusiano mazuri ni kama geti la kufungulia maendeleo. Tunapaswa kuendelea kuimarisha mshikamano na umoja wetu kama Watanzania kwa sababu maendeleo yanapatikana pale ambapo jamii inaishi kwa maelewano,” alisema.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali ikiwemo NSSF, WCF, OSHA na taasisi nyingine zinazotoa huduma za kijamii, ambapo alieleza kuridhishwa na ubora wa huduma zinazotolewa pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuwahudumia wananchi.
Alisema wananchi wanaotembelea maonesho hayo wanapata fursa ya kufahamu haki zao, kupata huduma za kijamii na kujionea maboresho yanayofanywa na taasisi za Serikali katika kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Aliwataka wananchi ambao bado hawajafika kwenye mabanda ya Ofisi ya Waziri Mkuu kutembelea maeneo hayo ili kujipatia elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa manufaa ya jamii.

