NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika nyanja za kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia, bado kuna haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema kiwango cha biashara kilichopo kwa sasa hakilingani na fursa kubwa za kiuchumi zilizopo nchini Tanzania na Namibia, hivyo kuna ulazima wa kuongeza juhudi katika biashara, uwekezaji na sekta nyingine za maendeleo ili wananchi wa nchi hizo wanufaike zaidi na uhusiano wao wa kihistoria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais Samia amesema ujio wa kiongozi huyo nchini kwa mara ya pili ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja unaonesha dhamira thabiti ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliojengwa na waasisi wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Dkt. Sam Nujoma.
Amebainisha kuwa Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Namibia, kupitia Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU Liberation Committee) iliyokuwa na makao yake makuu nchini Tanzania.
Rais Samia amesema historia hiyo imeweka msingi imara wa uhusiano wa karibu unaoendelea kushuhudiwa kati ya Tanzania na Namibia hadi leo.
Ameongeza kuwa Rais Nandi-Ndaitwah ana uhusiano wa kipekee na Tanzania kutokana na kuishi nchini hapa katika miaka ya 1980 na hata kufunga ndoa yake akiwa nchini, jambo linaloimarisha zaidi ukaribu wake na Watanzania.
Amesema katika mazungumzo yao, viongozi hao walikubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati, ikiwemo biashara, uwekezaji, usalama, madini, mafuta na gesi, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa mataifa hayo.
Aidha, Rais Samia ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Rais wa Namibia kuambatana na ujumbe wa wafanyabiashara katika ziara hiyo, akisema hatua hiyo itafungua fursa mpya za kibiashara, kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi na kuongeza uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika uchumi wa buluu, sekta ya mafuta na gesi pamoja na mifugo, ambapo Namibia imepata mafanikio makubwa na inaweza kushirikiana na Tanzania kwa kubadilishana uzoefu na teknolojia za kisasa.
Katika sekta ya elimu na utamaduni, Rais Samia alisema Namibia imeonesha nia ya kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuomba walimu wa Kiswahili kwa ajili ya kuwafundisha watumishi wa serikali na taasisi mbalimbali.
Akihitimisha, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kutumia kikamilifu rasilimali na fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wake.
Kwa upande wake Rais Nandi-Ndaitwah, amesema kuwa ziara hiyo ya kitaifa inalenga kuimarisha na kuhuisha mahusiano ya kihistoria na kidugu yaliyopo kati ya Tanzania na Namibia, mahusiano yaliyojengwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Dkt. Sam Nujoma.
Rais Nandi-Ndaitwah amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kugeuza mshikamano wa kisiasa uliodumu kwa miaka mingi kuwa ushirikiano wa kiuchumi wenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Amesema viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, huku wakisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya urasimu vinavyozuia bidhaa, mitaji na huduma kusafiri kwa urahisi kati ya nchi hizo mbili.
“Tunahitaji kuona ushirikiano wetu wa kidiplomasia ukizalisha ajira, kuongeza biashara na kuboresha maisha ya wananchi wetu,” amesisitiza
Aidha wamejadiliana kuhusu ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, uchumi wa buluu, maendeleo ya vijana, utamaduni na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa Rais huyo, Namibia na Tanzania zimekubaliana kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa makubaliano yaliyopo kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Commission of Cooperation) ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Amesema Mawaziri na wataalamu kutoka nchi hizo mbili wameelekezwa kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwa kuondoa vikwazo vilivyopo na kuhakikisha mikataba inayosainiwa inaleta matokeo halisi kwa wananchi.
Katika kuimarisha ushirikiano huo, Tanzania na Namibia zimesaini makubaliano katika sekta za ulinzi, biashara na maendeleo ya biashara ndogo na za kati, huku pia zikihamasisha ushirikiano wa watu kwa watu kupitia makubaliano kati ya Manispaa ya Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund ya Namibia.
Rais Nandi-Ndaitwah amewataka wafanyabiashara wa Tanzania na Namibia kutumia fursa zilizopo kuanzisha ubia na uwekezaji wa pamoja, akisisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi.
Amesema ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Namibia kwa lengo la kujenga mahusiano ya moja kwa moja na wafanyabiashara wa Tanzania na kuchochea biashara kati ya nchi hizo mbili.
Katika masuala ya kikanda na kimataifa, Rais huyo ameeleza Tanzania na Namibia zinaendelea kushirikiana katika kuimarisha umoja wa Afrika, amani na utulivu wa kikanda pamoja na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo wa amani, usalama na mshikamano miongoni mwa mataifa ya Afrika.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Nandi-Ndaitwah amesema Tanzania itaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha yake kutokana na kumbukumbu alizojijengea alipokuwa akiishi nchini humo kabla ya Namibia kupata uhuru.
“Niliishi Tanzania kwa miaka sita na sikuwahi kujisikia kuwa niko mbali na nyumbani. Hata baada ya Namibia kupata uhuru, mara nyingi ninapohitaji sehemu ninayoiona kama nyumbani, ninajikuta nikirejea Dar es Salaam,” amesema.
Amemshukuru Rais Samia kwa kumualika kufanya ziara hiyo ya kitaifa na kueleza matumaini yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Pia amemkaribisha Rais Samia kutembelea Namibia tena, akisema ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya mataifa hayo mawili unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tuna wajibu wa kutekeleza matarajio ya wananchi wetu. Tumejizatiti kuhakikisha tunalinda na kuendeleza urithi wa viongozi wetu waasisi kwa manufaa ya watu wa Namibia na Tanzania,” amesema.

