NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka Maofisa Tawala na Rasilimali Watu nchini kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ili kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Kikwete alitoa wito huo jana wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu uliofanyika katika Ukumbi wa Jenerali Mabeyo jijini Dodoma.
Mkutano huo umewakutanisha Maofisa Tawala na Rasilimali Watu kutoka wizara, idara, taasisi za serikali zinazojitegemea pamoja na mamlaka za serikali za mitaa kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali za taaluma yao na kuweka mikakati ya namna bora ya kukabiliana nazo.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kikwete alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano kati ya ofisi za washiriki na Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, aliwataka kutumia kikamilifu mifumo ya kidijitali na teknolojia za mawasiliano zilizotengenezwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora serikalini.
Waziri huyo pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na usimamizi wake ambao umeendelea kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa umma na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utumishi wa umma kuwa ni pamoja na ujenzi na uboreshaji wa mifumo mbalimbali ya kiutumishi, upandishaji wa madaraja kwa watumishi pamoja na ulipaji wa madeni yanayotokana na mishahara na stahiki za likizo.
Mkutano huo wa mwaka unaandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na unatoa jukwaa kwa wataalamu wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayolenga kuboresha utendaji kazi katika sekta ya umma.







