NA MWANDISHI WETU,NJOMBE
MRADI mkubwa wa uzalishaji wa kokoto uliopo mtaa wa Kambarage kata ya Njombe Mjini, unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa kokoto na kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya Serikali katika Mkoa wa Njombe.
Mradi huo unaomilikiwa na mchimbaji mdogo wa madini ya ujenzi, Isaya Boniface, umefungwa mtambo mkubwa wa kusaga kokoto wenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 1,000 kwa siku kwa kushirikiana na kampuni ya India ya Shree Sonal Earth Ltd iliyotoa usaidizi wa kitaalam katika utekelezaji wake.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Boniface amesema uwekezaji huo utamaliza changamoto ya upatikanaji wa kokoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisafirishwa kutoka mikoa ya Iringa, Dodoma na Pwani, hususan Lugoba, kwa matumizi ya miradi mbalimbali ya ujenzi mkoani Njombe.
Amesema mradi huo utasaidia kupunguza gharama za ujenzi, kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza mzunguko wa fedha pamoja na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohitaji kokoto kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa, amesema mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji muhimu unaotarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia madini ujenzi.
Amesema kutokana na uwezo wa uzalishaji wa tani 1,000 za kokoto kwa siku, Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 2.3 kwa siku kupitia tozo za mrahaba na ada ya ukaguzi, huku makadirio ya mapato ya mwaka yakifikia kati ya shilingi milioni 400 hadi 600.
“Mkoa wa Njombe unaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa sekta ya ujenzi wa miundombinu, makazi na miradi ya Serikali, hivyo uwepo wa mradi huu utaongeza upatikanaji wa malighafi muhimu kwa utekelezaji wa miradi hiyo,” amesema Mhandisi Mlekwa.
Aidha, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuwawezesha kupata mikopo na vifaa vya uzalishaji.
Mhandisi Mlekwa ameongeza kuwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Njombe, ikiwemo mradi wa kiwanda cha chuma, itaongeza mahitaji ya kokoto na kufungua zaidi fursa za uwekezaji katika sekta ya madini ya ujenzi.









