NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kukuza biashara za taifa la Belarus ikiwemo Kituo cha Taifa cha Kukuza Mauzo ya Nje (National Export Promotion Center) cha nchi hiyo ili kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Akizungumza katika mkutano wa kibiashara uliowakutanisha wadau kutoka Tanzania na Belarus, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk. Latifa Khamis amesema ushirikiano huo utajengwa kwa karibu na kituo hicho kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya biashara.
Amesema kupitia ushirikiano huo, TanTrade itaweka mkazo katika kuwafungulia wafanyabiashara wa Tanzania njia za kuingia kwenye masoko mapya pamoja na kujenga daraja la mafanikio litakalowezesha kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuvutia fursa za biashara na uwekezaji zitakazowanufaisha wafanyabiashara na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho cha Taifa cha Kukuza Mauzo ya Nje cha Belarus, Mikalai Barysevich amesema wapo utayari kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji na Tanzania kwa lengo la kupanua fursa za kiuchumi na biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema kuna nafasi kubwa ya kuendeleza biashara na kupanua uwekezaji wa pamoja, akisisitiza kuwa hatua ya kwanza ni kwa mataifa hayo kufahamiana zaidi kuhusu bidhaa, huduma na teknolojia zinazopatikana kwa kila upande.
“Jukumu la taasisi za kukuza biashara ni kusaidia wafanyabiashara kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja yatakayorahisisha biashara na kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi. Belarus imefika Tanzania ikiwa na utayari wa kushirikiana, tupo tayari kwenda mbali katika ushirikiano huo kulingana na utayari wa Tanzania,” amesema
Aidha, amesema Belarus ina fursa nyingi katika uzalishaji wa bidhaa pamoja na teknolojia ambazo ziko tayari kushirikiana na Tanzania ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.
Hata hivyo amesema kuwa Belarus ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mashine za kilimo duniani, ambapo kila trekta moja kati ya kumi zinazotumika duniani hutoka nchini humo, huku mashine moja kati ya sita za uvunaji pia ikizalishwa Belarus.
Amesema nchi hiyo inaongoza duniani katika utengenezaji wa malori makubwa ya migodini yenye uwezo wa kubeba hadi tani 450, teknolojia ambayo inaweza kuwa muhimu kwa nchi za Afrika zenye sekta kubwa ya madini.
Katika sekta ya kilimo, amesema Belarus ina uwezo wa kuzalisha mashine mbalimbali zinazoweza kutumika katika mazingira tofauti ya hali ya hewa, akitolea mfano mafanikio ya matumizi ya mashine hizo nchini Zimbabwe ambayo yamesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao.
Amesisitiza kuwa Belarus inaona nafasi kubwa ya kushirikiana na Afrika katika sekta za viwanda, kilimo, madini na teknolojia, akiahidi kuwa nchi hiyo iko tayari kutoa msaada wa kiufundi na uwekezaji ili kuchangia maendeleo ya bara hilo.




