NA MWANDISHI WETU,HOLILI, KILIMANJARO
MAHAKAMA ya Wilaya ya Rombo mkoani hapa imemuhukumu fundi bomba wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (ROMBOWSSA) Hemrod Ngunga kwa kosa la kushawishi kuomba rushwa ya Sh.20,000 /-kutoka kwa mteja ili aweze kumrejeshea mita zake zilizokuwa zimeibiwa maeneo ya Holili.
Kesi hiyo iliyotolewa maamuzi oktoba 15 mwaka huu na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo Innocent Nyella, kosa hilo la jinai namba 9081/2025 ni kinyume cha Sheria chini ya vifungu vya 15 (1)(a)(b)( 2) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022.
Kwa upande wa Mawakili wa Serikali Furahini Kibanga na Anorld Mafwele waliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa Ngunga akiwa Fundi Bomba ROMBOWSSA alishawishi, aliomba na kupokea hongo ya kiasi cha Sh. 20,000 hivyo Mahakama imemkuta mshtakiwa na hatia na kumuamuru kulipa faini ya Sh. 300,000/- au kwenda jela miaka mitatu.
Hata hivyo,Mshtakiwa ameshindwa kulipa faini hivyo amepelekwa rumande.

