NA ASHRACK MIRAJI,SAME,KILIMANJARO
MKUU wa Wilaya ya Same,Kasilda Mgeni, amewatakia heri wanafunzi wa darasa la saba walioanza rasmi Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi, huku akielezea matumaini yake kuwa Wilaya ya Same itafanya vizuri kitaifa.
Akizungumza leo Septemba 10,2025 ofisini kwake mjini Same, Mgeni aliwapongeza wanafunzi kwa hatua waliyofikia na kuwataka kujiamini na kusoma kwa umakini ili kufanikisha ndoto zao.
“Leo ni siku kubwa kwa watoto wetu. Ni siku ya kupima jitihada zao na za walimu wao. Nawapongeza kwa kufika hapa na nawatakia kila la heri. Tunaamini kuwa Same tutaibuka kidedea kwa kufanya vizuri kitaifa,” amesema Mgeni.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa maandalizi yamefanyika vizuri, huku akiwataka wanafunzi kufuata maadili ya mitihani na kuepuka vitendo vyovyote vya udanganyifu.
Ametoa wito kwa walimu na wasimamizi kuhakikisha mtihani unafanyika kwa utulivu na haki kwa wote.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wazazi, walezi, walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha maandalizi ya mitihani hiyo.
“Tunaishukuru jamii kwa kujitokeza kuwasaidia wanafunzi – iwe ni kwa chakula, usafiri, au kuwapatia mazingira tulivu ya kujisomea. Ushirikiano huu umeonyesha namna gani elimu ni ajenda ya pamoja,” ameongeza Mgeni.
Mkuu huyo pia aliwahimiza wanafunzi kuendelea kuwa watulivu katika siku zinazofuata, kula vizuri na kupumzika vya kutosha ili waweze kuendelea na mitihani kwa ufanisi.
Mitihani hiyo ya Taifa kwa darasa la saba inatarajiwa kuendelea kwa siku mbili kuanzia leo, ikihusisha masomo mbalimbali ya msingi kama vile Kiswahili, Hisabati, Sayansi, Kiingereza na Maarifa ya Jamii.