NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kuwa Agosti 9 hadi 27 mwaka huu itaanza utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais.
Hayo yamebainishwa leo Agosti Mosi,2025 na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima wakati wa mkutano wa kitaifa wa tume hiyo na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kailima amesema Agosti 27, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wagombea udiwani.
“Agosti 28 hadi Oktoba 28,2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara na Agosti 28 hadi 27, 2025 kitakuwa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema na Oktoba 29, 2025 itakuwa ndiyo siku ya kupiga kura,” amesema Kailima
Aidha amesema Agosti 14 hadi 27,2025 kutakuwa na utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani.
Aidha Kailima amesema jumla ya taasisi na asasi 164 zimepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura.
Amesema kati ya asasi na taasisi hizo 161 zimepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa upande wa Tanzania bara na tatu kwa upande wa Zanzibar.
“Tume pia imetoa vibali kwa taasisi na asasi za kiraia 88 kwa ajili ya kutazama uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Kati ya hizo 76 ni za ndani ya nchi na 12 ni za Kimataifa,” amesema Kailima