NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
BALOZI wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia nchini Tanzania, Balozi Fekadu Beyene Ayana, ametembelea Banda la Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Katika Banda la TCCIA,Balozi alipokelewa na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TCCIA, Matina Nkurlu, ambapo walifanya mazungumzo kuhusu nafasi ya kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia kupitia ushirikiano wa kibiashara, viwanda na uwekezaji wa sekta binafsi.
Balozi Fekadu ameonesha kuvutiwa na mchango wa TCCIA katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kusimamia huduma muhimu kama utoaji wa Cheti cha Uasili (Certificate of Origin), ambacho ni kiungo muhimu katika kurahisisha biashara za kimataifa.
Amesema kuwa Ethiopia iko tayari kuimarisha ushirikiano na Tanzania kupitia majukwaa ya kibiashara, ushiriki wa maonesho na programu za kuwakutanisha wafanyabiashara wa mataifa haya mawili.
Kwa upande wake,Nkurlu alieleza kuwa TCCIA imejipanga kuimarisha majukwaa ya ushirikiano wa kibiashara na mabalozi wa nchi mbalimbali kwa lengo la kufungua masoko mapya kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
“Tunatambua nafasi ya Ethiopia kama mdau muhimu katika biashara za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. TCCIA iko tayari kushirikiana na Ubalozi wa Ethiopia katika kupanga mikutano ya biashara, maonesho ya pamoja na programu za kuwakutanisha wafanyabiashara wa pande zote mbili,” amesema.