*WANANCHI WAISHUKURU WIZARA YA FEDHA KWA KUWAFUNGUA MACHO
NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WIZARA ya Fedha imeendelea kupongezwa kwa utoaji wa elimu yenye uhalisia na maisha ya wananchi katika masuala ya fedha na uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na matumizi bora ya fedha katika kuchochea maendeleo.
Hayo yameelezwa na ujumbe wa Shirika la World Vision Tanzania Mkoa wa Tanga wa mradi wa utunzaji mazingira, ukiongozwa na Swalehe Mwachuo, ulipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Mwachuo amesema kuwa wamevutiwa na elimu kuhusu Sera za Fedha na elimu ya huduma ndogo ya fedha ambayo inauhalisia kwa wajumbe wengi wa mradi huo na maeneo walikotoka.
Amesema kuwa, ujumbe uliotembelea Banda la Wizara ya Fedha umetoka Mkoani Tanga katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Handeni na Kilindi ambao umekuja kupata elimu ya kazi zinazofanywa na Wizara ya Fedha hususani zilizo na manufaa ya moja kwa moja kwa wajumbe hao.
Amesema wajumbe hao watapeleka taarifa kwa wananchi wengine kuhusu Sera za fedha na namna ya kuepukana na mikopo umiza, kukopa kwa malengo na kutotumia fedha za mikopo kwenye matumizi yasiyo na faida.
Mwachuo amesema kuwa wamejifunza kuwa fedha za mkopo sio za mkopaji bali faida ndio ya mkopaji hivyo ni vema kutumia fedha ya mkopo kuzalisha ili kupata faida.
Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kupitia Idara na Vitengo lakini pia Taasisi zilizo chini ya Wizara, wanaendelea kuwakaribisha watanzania kufika katika Banda la Wizara hiyo ili waweze kuwahudumia.