NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
ZAIDI ya Wafanyabiashara 20 wa Jimbo la Shandong Jamhuri ya Watu wa China wakiongozwa na Mtafiti wa ngazi ya juu wa Idara ya biashara ya Nje ya ‘Shandong Provincial Commerce Bureau’ Zhou Ying wamekutana na kuzungumza na Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja Makao Makuu ya Chemba hiyo jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara ya wafanyabiashara hao ni kujifunza kuhusu mazingira ya biashara nchini Tanzania pamoja na kutafuta fursa za ubia na uwekezaji kwa kushirikiana na TCCIA.
Akizungumza katika kikao hicho, Minja ameeleza kuwa Tanzania ina mazingira bora ya biashara na sera rafiki kwa wawekezaji pamoja na nafasi ya kipekee ya kijiografia inayowezesha kufikia masoko ya Afrika Mashariki, Kati, na soko kubwa la pamoja la Afrika (AfCFTA).
“Tanzania imejipanga kuwakaribisha wawekezaji kwa sera thabiti na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Kupitia TCCIA, tunatoa huduma zinazowawezesha wawekezaji kupata taarifa, kuwaunganisha na wafanyabiashara wa ndani, pamoja na utoaji wa nyaraka muhimu kama vyeti vya Uasili wa bidhaa yaani Certificate of Origin,” amesema Minja.
Ameongeza kuwa TCCIA ina historia nzuri ya ushirikiano na wawekezaji kutoka China huku akitolea mfano wa ushirikiano uliopo na EACLC, wamiliki wa soko kubwa la biashara Afrika Mashariki lililopo Ubungo,jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Ying amesifu kazi inayofanywa na TCCIA katika kukuza biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
“Tumevutiwa sana namna TCCIA inavyosaidia kuimarisha biashara kati ya Tanzania na mataifa ya nje. Mazingira ya uwekezaji hapa nchini ni ya kuvutia hivyo basi tunatarajia kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu,” amehitimisha Ying