NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WMA imesema ipo mbioni kutengeneza mifumo kwaajili ya kudhibiti mafuta
Mifumo hiyo itahakikisha mwenendo mzima na hatua ya mafuta yanapoingia,yanapotoka na yanapohifadhiwa .
Hayo yamebainishwa na Meneja wa WMA Kitengo cha Bandari Alfred Shungu wakati wa mahojiano maalumu katika Kipindi cha Kiss Ripoti kinachorushwa na kituo cha radio cha Kiss Fm cha jijini Dar es salaam leo jioni ya Julai 4,2025
“Wakala wa Vipimo tupo mbioni kutengeneza mifumo ambayo itasaidia udhibiti wa mwenendo wa mafuta
” Wengi wetu ni mashahidi juu ya suala la mafuta hivi sasa hakuna malalamiko kama hapo awali …hii ni kwasababu WMA ipo kazini inafanya kazi kubwa kuhakikisha suala la vipimo sahihi kwenye sekta ya mafuta linazingatiwa” amesisitiza Shungu.
Mbali ya hayo Shungu amesema kutokana na mafanikio hayo WMA inakwenda kuhakikisha mifumo inamaliza kabisa changamoto hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa WMA ,Veronica Simba amesisitiza kuwa Serikali yetu ni sikivu na ndio maana Wakala wa Vipimo wanafanya kazi kwa usahihi ili kukidhi matakwa na mahitaji ya walaji.
Akielezea juu ya umuhimu wa Wakala wa Vipimo ,Simba amejinasibu kuwa WMA ipo katika kila sekta muhimu ikiwemo afya ,Usafirishaji,Kilimo ,Chakula na Ujenzi .
“Mtu anapokwenda hospitalini akipimwa uzito Wakala wa Vipimo unahusika moja kwa moja kwasababu uzito wake ndio utaamua Daktari anakupa dawa ya ujazo gani
“Kadhalika hata kwenye maduka ya vyakula na vitoweo nazungumzia buchani WMA pia tunahusika moja kwa moja kuzuia kupunjwa ” amesisitiza Simba.
Wakati huo huo Simba ametoa rai kwa watanzania kutoa taarifa kwa WMA iwapo kutakuwa na viashiria vya udanganyifu katika suala la vipimo katika maduka ya vyakula,mabucha vituo vya mafuta na maeneo mengine.
” Nisisitize tu kwamba ni haki ya kila raia kutoa taarifa kwa WMA pale anapoona vipimo vinavyotumika vina udanganyifu na kwa kufanya hivyo hatua dhidi ya mhusika zitachukuliwa kwa haraka kwasababu lengo ni kuondoa na kufuta kabisa udanganyifu katika vipimo” ameeleza Meneja Uhusiano na Mawasiliano huyo.
Aidha amewataka watanzania kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika katika vipimo ikiwemo mizani kuwa vina nembo ya WMA.