*AAHIDI USHIRIKIANO,HUDUMA BORA KWA WANANCHI
NA MWANDISHI WETU,TABORA
MKUU mpya wa Wilaya ya Tabora,Upendo Wella, aapishwa rasmi na kuahidi kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya hiyo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.
Katika hafla yenye heshima na uzito wa kiutawala iliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Wella ameapishwa rasmi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora.
Uapisho huo umefuatia uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko ya kiutendaji ndani ya utumishi wa umma.
Mara baada ya kula kiapo chake cha utii, Wella alitumia jukwaa hilo kumshukuru Rais kwa imani kubwa aliyoionyesha kwake kupitia uteuzi huo.
Alisema uteuzi huo si tu ni heshima binafsi, bali ni wito wa kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kujitolea, uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.
“Kuteuliwa kwangu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora ni heshima kubwa. Namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuniamini. Naahidi sitawaangusha Watanzania na nitatumikia kwa kujitoa, kushirikiana na kuhakikisha kila mwananchi anahisi uwepo wa serikali,” alisema Wella kwa msisitizo.
Kabla ya uteuzi huu, Wella alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, ambapo alionesha uwezo mkubwa wa kiutendaji, mshikamano wa kiutawala na usimamizi madhubuti wa shughuli za maendeleo. Uzoefu huu, alisema, unampa nguvu mpya ya kulihudumia vema eneo lake jipya la kiutawala.
Akizungumza mbele ya viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tabora na wilaya zake, Wella alitoa shukrani kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kuahidi kushirikiana na kila mmoja katika kuhakikisha wilaya hiyo inasonga mbele.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya kweli hayaji kwa mtu mmoja, bali kupitia mshikamano na ushirikiano wa pamoja baina ya viongozi na wananchi.
“Nimepokelewa kwa upendo mkubwa na najua nina familia mpya hapa Tabora. Nitaendelea kushirikiana nanyi, kuwasikiliza na kufungua milango ya mawasiliano ili kwa pamoja tuhakikishe huduma zinawafikia wananchi kwa wakati, kwa haki na kwa ubora unaostahili,” alihitimisha.